Rais wa Shirikisho la Michezo Tanzania (TFF), Wallace Karia, ametoa ujumbe mzito kwa wadau wa michezo kupitia mkutano wake na wahariri wa habari za michezo.

Katika hotuba yake, Karia amegusia mambo mengi ikiwemo kazi zilizofanywa na shirikisho hilo kwa kipindi cha miezi saba akiwa rais, mashindano ya ligi mbalimbali pamoja na program ya Taifa Stars, Ligi ya wanawake pamoja na mapato na matumizi kuhuisha uwazi.

Ifuatayo ni sehemu kubwa ya hotuba yake, tumeiweka ili uipate mstari baada ya mstari kumpima kiongozi huyu wa TFF ndani ya kipindi kisichozidi miezi nane:

Ndugu zangu, leo nitaongelea mambo makubwa mawili ili waTanzania wapate kufahamu kinachoendelea katika mchezo wa mpira wa miguu hapa nchini.

Moja nitaongelea kuhusu mambo ambayo tumeyafanya kwa kipindi cha miezi saba nilichokuwepo madarakani lakini la pili ni mambo yanayoendelea sasa hivi kwenye Shirikisho.

MAMBO AMBAYO TUMEYAFANYA KWA MIEZI SABA TOKA TUINGIE MADARAKANI

 HALI NA SHUGHULI ZA TAASISI:

Kwa Mazingatio ya Utekelezaji Makini na wa Maendeleo wa Shughuli za Taasisi Tulitambulisha Muelekeo na Dira ya TFF ambapo Kazi iliyo Mbele yetu ni Kuzitoa na Kuimarisha Utambuzi na Utekelezaji wake. Sasa ni wakati Tunajiandaa Kutoa baadhi ya Mipango yetu na kutoa Dira za Utekelezaji wake. Pamoja na Mipango hiyo Bado TFF tumekuwa Tukitekeleza Shughuli za Mpira katika Mgawanyiko wake na labda kwa kifupi kugusia Miongoni mwake.

Mashindano:

Tumeendesha mashindano mbalimbali kwa ufanisi mkubwa yakiwemo mashindano ya Azam Sports Federation Cup, Ligi ndogo ya Wanawake kwa ajili ya kupata timu za kupanda daraja,Ligi Kuu ya Wanawake hatua ya makundi na hatua ya nane bora inayoendelea,Mashindano ya soka la ufukweni kwa timu za vyuo vikuu,Mashindano ya  kimataifa ya soka la ufukweni yajulikanayo COPA DAR ES SALAAM.

Azam Sports Federation cup;

Mashindano hayo kwa msimu huu 2017/18 tumeyaendesha kwa ufanisi na umakini mkubwa tofauti na huko nyuma kwa kuhakikisha upangaji wa ratiba umekuwa wa wazi usio na upendeleo wowote ule hivyo kupunguza malalamiko,jambo lingine tulihakikisha timu zote zinapata stahiki zao kwa wakati na kiwango kilichopangwa,kadiri tunavyoelekea hatua za mwisho wa mashindano tutahakikisha changamoto zote zilizojitokeza huko nyuma tunakabiliana nazo na kuzitatua ili kuhakikisha mashindano hayo yanaisha vizuri.

Ligi kuu ya Wanawake;

Mwaka huu tulianza kucheza Ligi ndogo ya Wanawake kutafuta timu za kupanda Ligi Kuu ya Wanawake katika vituo vya Dar es salaam na Dodoma,ikafuatiwa na Ligi ya Wanawake katika kituo cha Arusha na Dar es Salaam ili kupata Timu 8 za kucheza hatua ya Nane bora ya Ligi hiyo.

Katika hatua ya makundiTFF ilizigharamia timu zote kwa asilimia 100 kuanzia malazi, usafiri, chakula, gharama za maadalizi ya timu na nauli ya kwenda na kurudi,ikiwa ni mara ya kwanza katika historia ya mpira wa miguu wa Wanawake kwa TFF kugharamia kwa kiwango hiki.

Katika hatua ya Nane bora ya  Serengeti Lite Women Premier League vilabu vyote vilishapewa fedha zao kwa ajili ya hatua ya kwanza ambayo imesimama kupisha maandalizi ya timu ya Taifa ya Wanawake(Twiga Stars) ambayo inajiandaa na mashindano ya kufuzu michuano ya Afrika kwa Wanawake ambapo tayari timu ya Taifa ipo kambini ikijiandaa na mchezo huo dhidi ya Zambia.

Taasisi iliendesha kwa mafanikio makubwa mashindano ya soka la ufukweni (Copa Dar es Salaam) kwa kuzialika timu za Uganda, Malawi, Zanzibar na wenyeji Tanzania bara ambazo tulizigharamia malazi, chakula na usafiri wa ndani.

PROGRAMU ZA TIMU ZA TAIFA:

Toka tumeingia madarakani, tumekuwa tunafanyia kazi program mbalimbali za maendeleo ya Timu za Taifa.

 Taifa Stars:

Tumekuwa tukiendelea na program mbalimbali za Timu ya Taifa za kuhakikisha inafuzu Fainali za kombe la mataifa Afrika 2019.

Kuhakikisha hili Taifa Stars ilicheza na Benin, Malawi, Botswana na wiki hii tunacheza na Algeria pamoja na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) katika kalenda ya mechi za kimataifa ya FIFA.

Ili kuongeza hamasa ya wachezaji tumeongeza posho ya ndani kwa asilimia 100 na asilimia 50 kwa posho za nje.

Kilimanjaro Stars:

Timu yetu ya Tanzania bara ilishiriki mashindano ya CECAFA yaliyofanyika nchini Kenya mwezi Desemba 2017, mbali na kushiriki ili ichukuwe kombe sababu nyingine ilikuwa ni kuendelea kupata mechi nyingi za kimataifa.

Timu ilicheza dhidi ya Rwanda, Kenya, Zanzibar na Libya, Tunaamini kwa wachezaji vijana waliokuwa sehemu ya kikosi hicho imewajengea uwezo katika soka la kimataifa.

Timu za Taifa za Vijana:

Katika eneo hili  tumekuwa na mpango wa muda mrefu kuhakikisha vijana wa timu zetu za Taifa za miaka chini ya 23, 20, 17 na 13 zinakuwa na maandalizi bora na kwa kuanzia toka tuingie madarakani tumekuwa na kambi za timu za vijana kila mwezi kwa kuwakutanisha siku 14 za mazoezi na kuwatafutia mechi za kirafiki za kimataifa.

Timu ya U23:

Timu ya Taifa chini ya miaka 23 ambayo ni kikosi cha pili cha timu ya Taifa kimeshaitwa kambini mara kadhaa na tumethibitisha kushiriki mashindano ya Olimpiki ambayo fainali zake zitafanyika nchini  Japan, lengo ikiwa ni kuhakikisha tunawapatia vijana hawa mechi nyingi za kimataifa ili wawe tayari.

Timu ya Vijana U20:

Timu ya Vijana U20 ambapo jana ilicheza na Morocco na Jumatano itacheza na Msumbiji, ikiwa ni maandalizi ya mechi dhidi ya timu ya vijana chini ya miaka 20 ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Watu wa Congo(DRC) ikiwa ni mchezo wa kufuzu fainali za Vijana Afrika chini ya miaka 20.

Timu ya Vijana U16:

Timu hii nayo imekuwa ikiingia kambini kila mwezi na hata sasa hivi ninavyozungumza na nyinyi, timu hii ipo kambini ikijiandaa kwa mashindano ya CECAFA na tunafanya jitihada za kuhakikisha inapata mechi mbili za kirafiki za kimataifa kabla haijaenda Burundi.

Timu hii ndiyo ambayo itashiriki fainali za Afrika chini ya miaka 17 zitakazofanyika hapa nchini mwaka 2019.

Baada ya kutoka Burundi itakuwa na program maalum kwa ajili ya kujiandaa kwa mashindano mengine ya kufuzu AFCON U17, 2019 ambayo yatafanyika nchini mwezi Agosti ambayo lengo ni kupata mwakilishi wa CECAFA na vijana wetu watashiriki kama wenyeji. TFF imeamua kushirikisha Timu yenye Umri mdogo zaidi kwa u17 bila ya kujali Matokeo zaidi ya Ujenzi wa timu kwa kuandaa timu moja katika matukio yote haya ili kuiweka tayari kwa Mashindano ya u17 ya 2019 mwakani ambapo vijana hawa ndio watakuwa rasmi u17

Timu ya Vijana ya U13:

Timu ya Vijana ya U13 katika kutafuta namna ya Kuwaimarisha vijana  hawa baada ya Utambuzi na Uteuzi wa timu imepata nafasi ya  kushiriki mashindano ya kirafiki ya vijana chini ya miaka 13 yatakayofanyika nchini Ubelgiji mwezi Agosti 2018,Tayari orodha ya kwanza ya wachezaji 69  waliopatikana katika mashindano ya shule za msingi (UMITASHUMITA) ipo TFF na idara ya ufundi inaandaa utaratibu wa kuwaita pamoja na kupata michezo ya kirafiki dhidi ya Zanzibar kwa ajili ya kupata kikosi cha pamoja cha Tanzania.

Timu ya Taifa ya Wanawake U20:

Tumeanza kuandaa kikosi cha Vijana cha timu ya taifa ya Wanawake U20 ili kuwa na kikosi bora cha Twiga Stars kilichoandaliwa kwa muda mrefu na tayari ilishacheza michuano ya kufuzu fainali za vijana za Afrika chini ya miaka 20 na kutolewa na Nigeria.

Baadhi ya wachezaji wa timu hii wamepandishwa kikosi cha wakubwa na sehemu kubwa wanacheza Ligi Kuu ya Wanawake kupitia vilabu mbalimbali.

Tutaendelea na utaratibu wa kuwaita kambini kila wakati kutakapokuwa na nafasi ili kuzidi kuimarisha kikosi.

Twiga Stars:

Kikosi cha Twiga Stars kimeingia kambini kwaajili ya maandalizi ya mashindano ya kufuzu fainali za Africa kwa Wanawake zitakazofanyika nchini Ghana baadaye mwaka huu.

Twiga Stars inakabiliwa na mchezo dhidi ya Timu ya Taifa ya Zambia utakaochezwa Aprili 4,2018 Uwanja wa Taifa na marudiano kuwa Aprili 8,2018 nchini Zambia.

MAPATO NA MATUMIZI

 MAPATO

Katika kipindi cha miezi Saba(7),Shirikisho limefanikiwa kukusanya kiasi cha Tzs 3,670,397,199.00 kutoka katika vyanzo vyake mbalimbali  ambavyo ni pamoja na mapato kutoka kwa wadhamini Tzs 2,295,472,151 sawa na 62.5%ya mapato yote, makusanyo ya viingilio uwanjani Tzs 378,139,866 sawa na10.3%. 27.2% ilitokana na Fedha kutoka CAF na FIFA.

MATUMIZI

Katika kipindi hiki Shirikisho lilitumia kiasi cha Tzs 3,752,001,171.00. Sehemu kubwa ya matumizi yalielekezwa kwenye usimamizi wa ligi mbalimbali pamoja na kuandaa timu za taifa ambapo jumla ya Tzs 2,409,150,732 sawa na 64% ya matumizi yote zilitumika.

Asilimia 36 ya Fedha zilizobaki ilitumika kulipia madeni ya Taasisi, Kulipa mishahara ya wafanyakazi, kusaidia mikoa katika maeneo ya miundo mbinu, kuwajengea uwezo wafanyakazi pamoja na kuendesha mafunzo mbalimbali.

Kama Rais wa TFF sijapokea HOJA wala USHAURI wala MAPENDEKEZO yoyote kutoka kwa Wajumbe wangu katika Ngazi zote kuhusiana na Matumizi ya Taasisi, Nasikitika kama kuna anayedai amehoji sijui wapi kwa kuwa kama Rais sijapokea hoja yoyote wala kuwasilishwa katika kikao cha Kamati ya Utendaji iliyopita ambayo Taarifa ya Kamati ya Fedha iliwasilishwa nakupokelewa na kupitishwa na Kamati ya Utendaji.

MADENI

Katika kipindi hiki,Shirikisho lilianza zoezi la kutathmini madeni iliyoyarithi kutoka kwenye Uongozi uliopita, ambapo deni hilo linafikia Tzs 2,172,000,000linalodaiwa na watoa huduma mbalimbali, wafanyakazi,wachezaji na makocha.

Asilimia kubwa ya deni hili lilitokana na malimbikizo ya deni la TRA, Workers Compensation Fund na NSSF ambalo lililimbikizwa kwa zaidi ya miaka miwili.

Shirikisho lilifanikiwa kulipa deni lote la michango ya wafanyakazi NSSF jumla ya Tzs 88,000,000 zilizokuwa hazijalipwa kipindi cha miaka miwili, na lilifanya majadiliano na Mamlaka ya Mapato Tanzania kuhusu ulipaji deni la kodi linalofikia Tzs 1,077,000,000, ambapo jumla ya Tzs 315,000,000 zimelipwa nakiasi kilichobaki tumekubaliana kitalipwa kwa awamu kadhaa mpaka deni lote litakapomalizika.

Pia shirikisho limefanikiwa kupunguza mishahara kwa wafanyakazi kutoka Tzs  85,063,092.00 mpaka kufikia 50,000,000.00 baada ya kupunguza idadi ya wafanyakazi kutoka 44 mpaka 21.

Baada ya kuingia madarakani tulifanya majadiliano na makocha wa timu za Taifa kuhusu uhalisia wa malipo yao na kufanikiwa kuokoa zaidi ya dola laki mbili(USD 200,000) kwenye mikataba yao na fedha zilizookolewa zitasaidia shughuli nyingine za mpira wa miguu.

 

Video: Musiba awataka Watanzania wasikubali kutumika
Azam FC kujipima kabla ya kuwavaa Mtibwa Sugar