Wizara ya Afya imeanzisha huduma ya kujipima VVU mahala pa kazi ili kurahisisha upatikanaji wa huduma hiyo kwa Watumishi makazini hasa Wanaume, ambapo hadi kufikia mwezi Desemba 2022 jumla ya watu 96,231 wamepatiwa huduma hiyo.
Naibu Waziri wa Afya Dkt. Godwin Mollel ameyasema hayo jijini Dodoma wakati akiwasilisha taarifa kuhusu uhuishaji na majumuishi mbele ya kamati ya kudumu ya Bunge ya masuala ya UKIMWI.
Amesema, “Wizara imeanzisha huduma ya kujipima VVU (JIPIME) mahala pa kazi ili kurahisisha upatikanaji wa huduma ya vipimo vya VVU kwa Watumishi sehemu za kazi hususani Wanaume, hadi kufikia Desemba 2022 watu wapatao 96,231 wamepatiwa huduma ya JIPIME mahala pa kazi.”
Dkt. Mollel amesema hadi kufikia Desemba 2022 jumla ya Vijana balehe 47,705 (Wavulana 20,329 na Wasichana 27,376), walifikiwa katika Shule zipatazo 103 kupitia kampeni ya Kipepeo, inayotarajiwa kufanyika mwaka 2023 katika mikoa ya Morogoro, Tanga, Geita, Singida na Dodoma.