Mahakama nchini Saudi Arabia imewahukumu adhabu ya kifo watu watano kutokana na mauaji ya mwanahabari mkosoaji Jamal Khashoggi ya mwaka wa 2018 mjini Istanbul.
Mwendesha mashitaka mkuu wa Saudi Arabia amesema watu wengine watatu wamepewa vifungo vya jumla ya miaka 24 huku akibainisha mauaji hayo yalikuwa ni sehemu ya “operesheni haramu” na kuwashtaki watu 11 ambao hata hivyo majina yao hayakuwekwa wazi.
Amesema Saud al-Qahtani, mshauri wa zamani wa ngazi ya juu wa Mwanamfalme wa Saudi Arabia, alichunguzwa lakini hakushitakiwa na aliachiwa huru.
Mwandishi huyo aliyekuwa na miaka 59 alifikwa na umauti wakati akiishi Marekani na kuandika maoni kwenye gazeti maarufu la Washington Post.
Mara ya mwisho kounekana akiwa hai ilikuwa Oktoba 2, 2018 akiingia kwenye ofisi ndogo za ubalozi wa Saudia ili kuchukua karatasi zake za talaka, akiwa mbioni kumuoa mpezi wake wa Kituruki Hatice Cengiz.
Naibu mwendesha mashtaka wa Saudia, Shalaan Shalaan aliwaambia wanahabari Novemba 2018 kuwa mauaji yaliamriwa na mkuu wa “timu ya mapatano” iliyotumwa Istanbul na mkuu msaidizi wa idara ya usalama wa taifa ya Saudia kwa kazi ya kumrejesha Khashoggi nyumbani.
Wachunguzi pia walifikia hitimisho kuwa Khashoggi alifungwa kwa lazima kisha kukabwa koo na kamba kabla ya kudungwa sindano lukuki za dawa ambazo zilipekea kifo chake.
Baada ya hapo mwili wake ulikatwa katwa vipande na kukabidhiwa kwa mshirika wa kituruki nje ya ubalozi na mabaki hayo hayajapatikana tena.