Kocha mkuu wa Kaizer Chiefs, Gavin Hunt amezungumzia mipango yake juu ya jinsi anavyotarajia kumaliza matumaini ya Simba SC kurejea katika mchezo wa mkondo wa pili wa robo fainali ya Ligi ya Mabingwa kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa.
Simba SC watakuwa wenyeji wa Kaizer Chiefs kesho Jumamosi (Mei 22), katika Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es salaam, huku wakihitaji ushindi wa mabao matano kwa sifuri ama zaidi, ili kujihakikishia nafasi ya kutinga hatua ya Nusu Fainali.
Gavin Hunt amesema: “Ningejuta sana katika dakika 10 zilizopita ni kwamba hata matokeo yangeisha kwa bao 4-1, wangeweza kupata matumaini. Kwa hivyo, ilikuwa furaha kubwa kumaliza na bila kuruhusu bao,”
“Nadhani tutajaribu, ikiwa tunaweza kufunga bao moja ugenini basi ni kweli tutakuwa moja kwa moja katika nusu fainali, nina maanisha hiyo itakuwa kazi rahisi kufanywa na vijana wangu.”
“Nimekuwa Tanzania hapo awali, tulicheza na Azam FC nchini Afrika Kusini na tulipokwenda kwao walibadilika ma kuwa timu tofauti kabisa, ilionekana kama walikuwa na wachezaji 12-13 uwanjani.
“Kwa hivyo, dhidi ya Simba tunatarajia utakuwa mchezo tofauti kabisa; ni timu kubwa yenye uwezo mkubwa wa kumiliki mpira lakini sisi tuna faida ya bao 4-], tutafanya kazi kwenye mazoezi na kujaribu kuboresha vitu tunavyoweza, ndio jambo tunaweza kufanya.”