Uongozi wa Klabu ya Simba umeweka wazi kuwa licha ya kupangwa na wapinzani wakubwa katika hatua ya Robo Fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika, Wydad Casablanca hawajamaliza mwendo wa mapambano watapambana kutimiza malengo yao.
Meneja wa Idara ya Habari na Mawasiliano wa Simba Ahmed Ally amebainisha kuwa kwenye mashindano makubwa ni lazima wakutane na wakubwa hilo haliwapi shaka kutokana na uimara walionao.
“Ni kweli tunakutana na mpinzani mgumu ambaye ni Wydad Casablanca hilo halitupi shaka na wale wanaofikiria mwendo tumemaliza waondoe kabisa akilini kama ikitokea tumepoteza basi hatuna cha kujilaumu kwa kuwa tumepambana kiasi cha kutosha.”
“Tunataka kuandika historia mpya barani Afrika kwa kumtoa Wydad Casablanca sisi Simba tunafurahi kupangwa na hawa tunaamini tunakwenda kufanya vizuri.”
“Wale wanaocheka kuona tumepangiwa Wydad hilo ni juu yao, sisi tunawafuata kwa nidhamu na tunajua wapo juu ila sisi tutafanya jitihada na maandalizi mazuri kwenye mechi ili kupata matokeo na kutinga hatua ya nusu fainali.” amesema Ahmed Ally
Mchezo wa kwanza Simba SC inatarajiwa kuanza nyumbani Dar es salaam katika Uwanja wa Benjamin Mkapa, kasha itacheza Aprili 21 ugenini mjini Casablanca nchini Morocco Aprili 28.