Balozi John William Herbert Kijazi amewahi kuwa mwakilishi wa Tanzania nchini India, Singapore, Sri Lanka, Bangladesh na Nepal mwenye makazi yake jijini New Delhi, India kuanzia mwaka 2007 – 2016 na hivyo kumfanya kuwa Mkuu wa Mabalozi wote wanaowakilisha Tanzania nje ya nchi.
Kabla ya kuwa balozi, Mhandisi Kijazi alikuwa Katibu Mkuu Wizara ya Ujenzi na baadaye Wizara ya Maendeleo ya Miundombinu kuanzia mwaka 2002 hadi 2006, baada ya kuteuliwa kuwa Balozi ndani ya Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa na hatimaye kupangiwa kituo cha New Delhi, India.
Kati ya mwaka 1996 hadi 2002, Kijazi alikuwa Mhandisi Mwandamizi wa Ujenzi wa Barabara ndani ya Wizara ya Ujenzi kabla ya kupandishwa cheo na kuwa Mkurugenzi wa Barabara za Mikoa ndani ya Wizara hiyo hiyo.
Balozi Kijazi alipata Shahada ya Sayansi ya Uhandisi wa Umma mwaka 1982 kutoka Chuo Kikuu cha Dar es salaam, na baadaye Shahada ya Uzamili katika Uhandisi wa Barabara Kuu kutoka Chuo Kikuu cha Birmingham, Uingereza mwaka 1992.
Agosti 21, 2020 aliteuliwa na Rais Magufuli kuwa Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dodoma kuchukua nafasi ya aliyekuwa Makamu Mkuu wa Chuo hicho Hayati Benjamin Mkapa ambaye alifariki Julai 2020.
Balozi Kijazi aliteuliwa kuwa Katibu Mkuu Kiongozi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Machi 6, 2016 na kuapishwa Machi, 7 2017, wadhifa ambao ameushikilia hadi umauti unamkuta Februari 17, 2021, akiwa katika Hospitali ya Benjamin Mkapa jijini Dodoma.
Balozi John Kijazi amemuoa Fransiscar Kijazi na pamoja wamejaliwa wa watoto watatu, David, Emmanuel na Richard Kijazi.