Kocha wa Mabingwa wa Soka nchini Sudan Al Hilal ‘Omdurman’ Florent Ibenge amesema anatamani kuwa na Kiungo Mshambuliaji kama Pape Ousmane Sakho na Beki Henock Inonga Baka.
Ibenge ametoa kauli hiyo ya matamanio baada ya kuwashuhudia wawili hao wakicheza kwenye mchezo wa Kimataifa wa Kirafiki jana Jumapili (Februari 05), Uwanja wa Benjamin Mkapa.
Kocha huyo kutoka DR Congo amesema Sakho ni mchezaji wenye kiwango cha hali ya juu sana, na amekua msaada mkubwa Simba SC, na ndio maana amekuwa akitumika kama mkombozi pale timu inapohitaji matokeo.
“Natamani sana kuwa na mchezaji kama Sakho, viongozi wa klabu yangu wakisema niwataje wachezaji ambao ninawahitaji kwa hapa Afrika kwa sasa ili tuwasajili sitakosa kuwataja Pape Sakho,”
“Hata Inonga ni beki bora sana kuwahi kumuona hapa Afrika, kwa hiyo ikitokea nikitakiwa kusajili beki nitapendekeza jina lake ili tumsajili.” amesema Ibenge
Kuhusu mchezo dhidi ya Simba SC uliomalizika kwa sare ya 1-1, Kocha Ibenge amesema: “Tangu kipindi cha kwanza sikubahatika kufahamu Simba SC inacheza mpira wa aina gani kwani sikuona Simba SC ikicheza soka ambalo nimezowea kuona Simba SC, ikicheza”
“Kipindi cha kwanza nilipanga kikosi kwa kulinda zaidi nikijuwa kuwa Simba Sc itaanza na mpira wao wa kila siku ila haikuwa hivo”
“Kipindi cha pili nikabadili mfumo ili kushambulia zaidi Simba SC nao wakafanya mabadiliko ambayo yalionesha makali yao, tukajikuta tunashambuliwa zadi ndipo kuridisha bao na kutaka kuongeza bao.”
“Kipindi cha pili niliona Soka bora sana kwa upande wa Simba SC, wana kikosi bora sana kina uwezo wa kufanya vizuri kimataifa naimani katika kundi lao wanao uwezo wa kumaliza nafasi ya pili ama ya kwanza.”