Sakata la wachezaji wa klabu bingwa Tanzania bara Young Africans kugomea kufanya mazoezi, tukio lililotokea Jumanne ya Septemba 19, limechukua sura mpya baada ya uongozi uliopo madarakani kushutumiwa vikali kuwa unahusika.
Shutuma hizo zimetolewa na Katibu wa Baraza la Wazee wa Klabu ya Young Africans, Ibrahim Akilimali ambaye amedai kuwa mgomo huo una mazingira ya kutengenezwa na kushauri ni bora wachezaji wangegomea kucheza mechi na siyo kugomea kufanya mazoezi.
Mzee Akilimali amesema anachoona kuna mpango wa kuwafanya wachezaji wagome kwa kuwa suala hilo limekuja siku moja tu tangu nahodha wa Yanga, Nadir Haroub ‘Cannavaro’ pamoja na bechi la ufundi walipokutana na aliyekuwa mwenyekiti wa klabu hiyo Yusuf Manji.
Akifafanua zaidi suala hilo, Akilimali alikuwa na haya ya kusema: “Mimi naamini hapa kuna kitu, haiwezekani wagome muda mfupi baada ya kuonana na Manji, labda wanataka kufanya hivyo kwa kuwa mimi nilimpinga Manji.
“Unajua mimi simchukii Manji wala naamini yeye hanichukii lakini kitendo cha mimi kupinga timu kukodishwa ndiyo chanzo.
“Hata huyu kiongozi wetu wa sasa, Clement Sanga naye ni tatizo kwa kuwa matatizo yametokea yeye akiwa katika mambo yake mengine, anatakiwa ashughulikie hili suala, kingine ninachojiuliza ni kuwa Sanga alizungumza na nahodha kisha muda mfupi baadaye tunaambiwa wachezaji wamegoma.
“Kwa nini wagome sasa hivi wakati timu imeenda kumuona Manji, hapo kuna kitu, walitakiwa wagomee mechi ili viongozi wafanya kazi kuwabembeleza wacheze na siyo kugomea mazoezi.”