Idadi ya watu waliofariki wakati wakisheherekea sikukuu ya Diwali katika ajali ya kuporomoka kwa daraja huko Gujarat nchini India imeongezeka kutoka watu 75 na kufikia hadi 132.
Vikosi vya jeshi la nchi hiyo, vimefanikiwa kuwaokoa watu 177 huku wengine kadhaa wakiwa bado hawajapatikana huku mamlaka zikibaini kuwa daraja hilo la watembea kwa miguu lililojengwa enzi za ukoloni katika wilaya ya Morbi, liliporomoka kwa kushindwa kustahimili uzito wa umati mkubwa wa watu.
Watu hao, wanaokadiriwa kufikia 500 na ambao walikuwa wakiadhimisha sherehe za kiimani za Diwali walikumbwa na tukio hilo baada ya nguzo zilizokuwa zinalishikilia daraja hilo kukatika.
Daraja hilo la Machchu, lililojengwa karibu miaka 150 iliyopita na lina urefu wa zaidi ya mita 200 na lilifunguliwa siku ya Jumatano baada ya kufungwa kwa miezi saba kwa ajili ya matengenezo.
Hata hivyo, lilifunguliwa kabla ya kupata idhini ya wakaguzi huku Waziri mkuu India, Narendra Modi akitangaza kuwa Serikali itazilipa familia za wahanga, wakati operesheni za uokozi zikiendelea.