Umoja wa Mataifa – UN, umesema vita vinavyoendelea kati ya majenerali wawili wa Sudan vinazidi kusababisha madhara mabaya kwa raia , huku idadi ya waliolazimika kuyahama makazi yao ikiongezeka maradufu.
UN inasema kuna wasiwasi kuwa mapigano tofauti ya kikabila yalisababisha vifo vya watu 16 kusini mwa nchi hiyo, na kundi lenye nguvu mashariki mwa nchi ambalo halijahusika katika vita, lilijitokeza na kuliunga mkono jeshi la taifa.
Shirika moja la uhamiaji linasema zaidi ya watu 700,000 wanasadikika kuyahama makazi yao na wengine waliohamishwa kutokana na mapigano tangu Aprili 15.
Idadi kubwa ya watu wanavuka mipaka kutoroka mzozo kati ya Mkuu wa Jeshi, Abdel Fattah al-Burhan, na Makamu wake wa zamani, Mohamed Hamdan Dagalo, ambaye anaongoza kikosi cha Rapid Support Forces – RSF.