Serikali nchini Burkina Faso, imesema idadi ya watu waliouawa katika shambulio lililofanywa na kundi linaloshukiwa kuwa ni la wanajihadi wenye msimamo mkali walio na uhusiano na Islamic state mjini Seytenga Jimbo la Sahel kaskazini mwa Burkina Faso, imefikia 79.
Kufuatia vifo hivyo, Rais wa mpito wa Burkina Faso, Luteni Kanali Paul-Henri Sandaogo Damiba, ametangaza kipindi cha saa 72 cha maombolezo ya kitaifa, ikiwa ni muda mfupi baada ya kupatikana kwa miili mipya 29.
Kulingana na agizo la Rais, maombolezo hayo ya kitaifa yameanza hii leo Juni 14, 2022 na yatamalizika siku ya alhamisi Juni 16, 2022 huku Umoja wa Ulaya (EU), ukilaani shambulio hilo na kusema idadi hiyo ya waliouawa inaweza kufikia watu 100.
“Maombolezo haya yatazingatiwa katika eneo lote la kitaifa, kwa kumbukumbu ya waathirika wa shambulio lililofanywa na watu wasiojulikana wenye silaha dhidi ya mji wa Seytenga, katika mkoa wa Séno, mkoa wa Sahel, wakati wa usiku wa Juni 11 hadi 12,” amesema Luten Dabima.
“Na katika kipindi hiki, bendera zitapeperushwa nusu mlingoti kwenye majengo yote ya umma na katika uwakilishi wa Burkina Faso nje ya nchi mambo ya sherehe maarufu na hafla za kiburudani ni marufuku hadi tutakapomaliza maombolezo,” amesisitiza Rais huyo wa mpito.
Naye Mkuu wa Diplomasia ya Ulaya Josep Borrell amesema mchakato uliotumiwa na kundi la kigaidi lililofanya shambulio hilo, kwa kunyonga kila mtu katika kijiji hicho ni wa kutisha na unapaswa kulaaniwa vikali na Mataifa yote.
Licha Luteni Kanali Damiba kuingia madarakani kwa kumpindua Rais Roch Marc Christian Kaboré, ambaye alishutumiwa kwa kutofanya kazi dhidi ya ukosefu wa usalama, mashambulizi ya vuguvugu hizi zenye mafungamano na al-Qaeda na Dola ya Kiislamu bado yamekwama.
Taarifa zinasema kuwa kwa kipindi cha miezi mitatu karibu raia zaidi ya 300 wameuawa wakiwemo na wanajeshi katika eneo hilo la kaskazini na mashariki mwa nchi ya Burkina Faso linayopakana na nchi ya Mali na Niger.
Tangu mwaka wa 2015, mashambulizi yanayohusishwa na wanajihadi yameua zaidi ya watu 2,000 na watu zaidi ya milioni mbili kukimbia nchini Burkina Faso.