Baadhi ya wachezaji wa kigeni wanaocheza ligi kuu ya soka Tanzania bara, wamenza kutoa maoni juu ya hoja ya Serikali kupitia Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo kupunguza idadi ya wachezaji wa kigeni.
Mshambuliaji Wa Kimataifa wa DR Congo David Molinga (Ndama) ametoa lake la moyoni Kuhusu idadi ya Wachezaji Wa kigeni Katika ligi ya VPL, ambapo amesema haoni tatizo la idadi kubwa ya wachezjai wa kigeni katika ligi ya hapa nchini ama lingi nyingine, suala kubwa hapo ni kuangalia ni vipi anavyofanya vizuri na kuzisaidia klabu zao.
Molinga ambaye ni kinara wa mabao Katika kikosi cha Young Africans msimu huu, ameongeza kuwa, wachezaji wa kigeni pia wamekua msaada mkubwa wa kuzisaidia klabu zao kwenye michuano ya kimataifa hususana katika bara la Afrika.
“Uwepo wa wachezaji kumi katika nchi fulani ambao wote wanafanya vizuri yani wana viwango bora na imara itafanya klabu kuwa bora katika maeneo mbalimbali yani kwenye ligi husika kwenye mashindano ya kimataifa pia.” Alisema David Molinga, ambaye alisajiliwa msimu huu akitokea FC Renaissance.
Kwa upende wa mshambuliaji kutoka nchini Zambia Obrey Chirwa ambaye Anakipiga Katika Klabu ya Azam FC, amesema matamanio yake ni kuendelea kuona wachezaji wa kigeni wanakua na viwango bora, na kuzisaidia klabu zao, sio kuwa mizigo.
Mshambuliaji huyo ambaye mwishoni mwa juma lililopita alisaini mkataba mpya wa kuendelea kuitumikia Azam FC kwa mwaka mmoja, amesema kila siku wachezaji wa kigeni wamekua wakizungumzwa kwa mazuri na mabaya, lakini anaamini sana kwa upande wa mazuri, hasa wanapotoa msaada.
Amesema haipendezi kwa mchezaji wa kigeni anaesajiliwa na kuja Tanzania kuonyesha kiwango duni, hivyo kwa upande wake anaamini idadi iliopo inatosha lakini izingatiwe ubora na uwajibikaji wa wachezaji wanaosajiliwa.
“Natamani sana kuona wachezaji wote wa kigeni tukiwa tunafanya Vizuri ili kuwapa upinzani wazawa Ambao nao watataka kuonesha ubora wao ambao utafanya timu na ligi kuwepo na ushindani Wa kuvutia”. Alisema Mshambuliaji wa Azam FC raia wa Zambia.