Baada kuwasambaratisha maafande wa Jeshi la Magereza (Tanzania Prisons) kwa kuwabamiza bao moja kwa sifuri kwenye uwanja wa Kumbukumbu ya Sokoine jijini Mbeya mwishoni mwa juma lililopita, wekundu wa Msimbazi Simba wametamba kuisasambua Lipuli FC katika mchezo wa mzunguuko wa wa 11 wa ligi kuu ya soka Tanzanai bara.
Mchezo huo utapigwa Jumapili ijayo kwenye Uwanja wa Chamazi Complex uliopo nje kidogo ya Jiji la Dar es Salaam, kutokana na Uwanja wa Uhuru kuwa na shughuli nyingine.
Kaimu makamu Rais wa Klabu ya Simba, Idd Kajuna amesema maandalizi ya kikosi chao yanaendelea kama kawaida kwenye Uwanja wa Chuo cha Polisi Kurasini.
kiongozi huyo alisema: “Tupo kwenye maandalizi makali kujiandaa na mchezo huo wa Jumapili dhidi ya Lipuli, ni mchezo mzuri na mgumu kwa sababu ligi ya msimu huu imejaa ushindani huwezi kuibeza timu yoyote ndiyo maana Simba na Azam tunalingana kwa pointi.”
Kajuna amesema wameupa umuhimu mkubwa mchezo huo kuhakikisha wanashinda kwani, wachezaji pamoja na benchi la ufundi wanajua ushindani uliopo hivi sasa na madhara ya kupoteza mchezo nini ambacho kitatokea.
Simba ipo kileleni mwa msimamo wa ligi hiyo kwa sasa ikijikusanyia pointi 22, sawa na Azam FC, lakini yenyewe ipo nyuma kwa idadi ya mabao na mabingwa watetezi Yanga wapo katika nafasi ya tatu kwa kujikusanyia pointi 20.