Inspekta Jenerali wa Polisi nchini Kenya,, Japhet Koome ametoa onyo kali dhidi ya wanaopanga kusababisha fujo wakati wa maandamano ya kila Jumatatu yaliyopangwa kufanywa na Muungano wa Azimio la Umoja, dhidi ya serikali
Kwa mujibu wa kituo cha habari cha Citizen, IG Koome alithibitisha kuwa hakuna mtu yeyote mwenye nia ya kusababisha fujo atakayeruhusiwa kuingia katikati mwa jiji na pia kuzuiwa kuondoka katika makazi yao husika.
Mkuu huyo wa Polisi, alithibitisha kuwa vikosi vya usalama vimejipanga vilivyo kwa ajili ya maandamano hayo na kwamba hawatakuwa na huruma kwa mtu yeyote atakayepatikana na “silaha za kushambulia” ikiwa ni pamoja na mawe, mapanga na rungu.
“Tuna wageni kutoka mataifa mengi ya kigeni na hatutaruhusu chochote kutokea katika mji wetu mkuu. Kila mtu ana haki ya kuingia katikati mwa jiji,” alisema Koome.
Aliongeza kuwa, “nina jukumu la kuhakikisha kwamba ninalinda maisha na mali na ninafanya vizuri sana. Sitalala kazini, kiwango chochote au hadhi uliyo nayo katika jamii. Nina magari ya kusafirishia ardhi ya kutosha kukupeleka jela na kuwa huko kwa maisha.”
“Tuko tayari kama polisi kuhakikisha kuwa kuna utulivu nchini kote kuanzia Nairobi. Kila Mkenya aendelee na kazi yake kesho. Letu ni kuhakikisha kila kona ya nchi hii iko salama. Hii ni nchi yetu. na ningewasihi sote tujivunie kuwa Wakenya.”
Aidha, amepuuzilia mbali nia ya maandamano hayo ambayo ni kuikemea serikali dhidi ya ughali wa maisha akibainisha kuwa maandamano hayo yana msukumo kamili wa kisiasa na yanapaswa kutatuliwa kisiasa badala ya kusababisha uharibifu katika taifa.