Viongozi kutoka mataifa ya Afrika Mashariki yanayounda Shirikisho la Maendeleo la Pembe ya Afrika (IGAD), wamekutana Jumapili Desemba 20, 2020, Djibouti kwa mkutano wa kilele, kujadili mzozo wa Tigray pamoja na mvutano kati ya Somalia na Kenya.
Mkutano huo mahususi kwa mazungumzo kujadili mchakato wa amani na usalama wa kanda hiyo, umehudhuriwa na Rais wa Djibouti Ismail Omar Guelleh, Uhuru Kenyatta wa Kenya, Mohamed Abdullahi wa Somalia na Waziri Mkuu wa Ethiopia Abiy Ahmed.
Katika mkutano huo Moussa Faki Mahamat, ambaye anaongoza Kamisheni ya Umoja wa Afrika amewahimiza wanachama wa IGAD kuisaidia Ethiopia kushughulikia mgogoro wa kibinadamu unaotokana na mzozo katika mkoa wake wa Tigray huku akizihizihimiza Kenya na Somalia  kutuliza mivutano kupitia njia ya mazungumzo.
Somalia ilivunja uhusiano wa kidiplomasia na Kenya mnamo Desemba 15, ikimshutumu jirani yake kwa kukiuka mipaka inayolinda uhuru wa taifa hilo.