Wanafunzi  564 waliofaulu Mtihani wa Kuhitimu Elimu ya Msingi mwaka huu kutoka halmashauri mbili mkoani Rukwa, hawakuchaguliwa kujiunga na kidato cha kwanza  awamu  ya kwanza kutokana na kukosekana kwa vyumba vya madarasa.

Hayo yameelezwa  na Mkuu wa Mkoa wa Rukwa, Joachim Wangabo wakati wa kutangaza uchaguzi wa wanafunzi wa kidato cha kwanza.

“Nafahamu kuwa wanafunzi 16,540 wamechaguliwa kujiunga Kidato cha Kwanza 2021 kwa awamu ya kwanza. Lakini pia wapo wanafunzi 564, kati yao wanafunzi 310 kutoka Manispaa ya Sumbawanga na 254 Halmashauri ya Wilaya ya Kalambo, ambao hawakuchaguliwa katika awamu hii kutokana na kukosekana kwa vyumba vya madarasa,” amesema Wangabo.

Aidha  Wangabo amewataka  mkuu wa Wilaya ya Kalambo,  na Mkuu wa Wilaya ya Sumbawanga kusimamia kikamilifu upatikanaji wa vyumba vya madarasa vinavyohitajika na wanafunzi waliokosa nafasi ili kabla ya Februari 28, mwakani wajiunge na kidato cha kwanza.

Ameeleza kuwa mkoa huo katika kata 27 hazina shule za sekondari, ambapo wilaya ya Kalambo zipo kata nane, Nkasi saba, Manispaa ya Sumbawanga mbili na Halmashauri ya Sumbawanga kumi.

Pia, amewataka maofisa elimu kuongeza ufuatiliaji wa taaluma shuleni ili kuhakikisha walimu wanafundisha kwa kufuata mitaala.

Pascal Wawa: Tunahimizana kupambana hadi mwisho
Kocha Sven aeleza Simba SC 'itakavyoipiga' FC Platinum

Comments

comments