Mkuu wa Jeshi la Polisi Nchini, IGP Simon Sirro amelaani vitendo vya mauaji vinavyofanywa na baadhi ya watu kwenye jamii, na kusema vitendo hivyo haviwezi kuvumiliwa.
IGP Sirro, ameyasema hayo Mkoani Iringa mara baada ya kukagua gwaride maalum, kujionea mazoezi ya mbinu za medani, na kusisitiza jinsi jeshi hilo lilivyojipanga kukabiliana na uhalifu nchini.
“Jeshi la Polisi litaendelea kuwachukulia hatua kali za kisheria watu watakaobainika kujihusisha na vitendo vya uhalifu hasa mauaji, na lazima wakikamatwa tutawafikisha Mahakamani,” amesema Sirro.
Akizungumzia matukio ya ubakaji na makosa ya kijinsia, IGP Sirro ameutaja Mkoa wa Iringa kuwa kinara wa matukio hayo, ikiwemo yale ya unyanyasaji wa kijinsia ambayo yanachangiwa kwa kiasi kikubwa na imani za kishirikina.
Aidha, IGP Sirro amesisitiza juu ya suala la ulinzi wa shirikishi kwa umma na kwamba Wananchi wanatakiwa kushiriki kwenye jukumu la ulinzi na vikundi vya ulinzi.
Kuhusu suala la maadili, IGP Sirro amewataka Askari wa Jeshi hilo kuwaheshimu Watanzania na kuhakikisha wanatenda haki kwa wananchi wanaowahudumia kama dhana ya usalama wa Raia inavyojieleza.