Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Freeman Mbowe huenda akafikishwa mahakamani na jeshi la polisi kwa kosa la uchochezi endapo itabainika kuwa shambulizi analodaiwa kufanyiwa katika makazi yake mkoani Dodoma lilikuwa la udanganyifu.
Hayo yamebainishwa na Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini, IGP Simon Sirro katika kipindi cha dakika 45 ITV, na kubainisha kuwa licha ya kuendelea na uchunguzi wa tukio hilo, bado hawajapata ushirikiano wa kutosha kutoka kwa Mbowe.
IGP Sirro amesema jeshi lililazimika kutumia nguvu, kumhoji dereva wa mwanasiasa huyo ambaye awali alikataa kufanya mahojiano bila sababu za msingi.
“Huyu dereva wa Mbowe kwanza alizuiliwa kuzungumza, hadi pale nilipopata taarifa hizo na nikawaagiza askari wahakikishe dereva huyo anazungumza na kueleza kilichotokea” amesema IGP Sirro.
Amebainisha kuwa askari waliwahoji majirani wa eneo hilo ili kubainisha kama walisikia kelele za Mbowe kuomba msaada, lakini majirani hao wanasema kuwa hawakusikia kelele zozote.
Aidha amesisitiza kuwa uchunguzi ukikamilika na ikabainika kuwa Mbowe alidanganya kuvamiwa na kuwa alianguka mwenyewe kwenye ngazi basi atashtakiwa.