Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan amewaapisha Viongozi wateule Ikulu, Chamwino jijini Dodoma hii leo Julai 20, 2022.
Viongozi hao, ni Inspekta Jenerali CAMILLUS MWONGOSO WAMBURA, kuwa Mkuu wa Jeshi la Polisi (IGP), na aliyekuwa Mkuu wa Jeshi la Polisi (GP) SIMON NYAKORO SIRRO, kuwa Balozi Wa Tanzania Nchini Zimbabwe.
Wengine, ni Balozi Luteni Jenerali MATHEW EDWARD MKINGULE, kuwa Balozi wa Tanzania nchini Zambia na Dkt. SULEIMAN HAJI SULEIMAN kuwa Balozi.
Akiongea mara baada ya uapisho huo, Rais Samia amemshukuru IGP mstaafu Simon Sirro kwa utendaji wake ndani ya Jeshi hilo na kusema nyakati zinabadilika hivyo mabadiliko ni lazima na kwamba anatarajia ataiwakilisha vyema Tanzania nchini Zimbabwe.
“Sera za Zimbabwe na Tanzania hazipishani sana tunafanana hivyo natarajia utatuwaklilisha vyema katika eneo hilo, asante kwa utumishi wako ndani ya Jeshi na kama tujuavyo mambo yanabadilika hivyo mabadiliko nayo ni lazima,” amesema Rais Samia.
Aidha, amesema anampongeza IGP mpya Wambura na kwamba anamtakia mema katika kutekeleza majukumu yake ndani ya Jeshi hilo huku akisema mabadiliko makubwa yatafuatia ili kufanya maboresho.
“Najua umefanya mengi ndani ya Jeshi hili hivyo natarajia utaendeleza mazuri yote katika majukumu yako mapya ndani ya jeshi hili na niseme mabadiliko makubwa yanakuja ndani ya jeshi hili,” amebainisha Rais.
Rais samia amesema, ni lazima kuangalia namna ambavyo utoaji vyeo umekuwa ukifanyika kwani kuna mapungufu na kutaka hatua hiyo iwe inafanyika kwa kuangalia taaluma na kuzingatia mafunzo kutokana na kutokuwepo kwa tofauti kati ya wanaostaafu na wanabakia ambao ni vijana.
“Unakuta anayestaafu mabegani hata tofauti na polisi vijana hili lazima liangaliwe na pia ni lazima kuangalia stahiki kwa kila nyanja ndani ya jeshi, ikiwemo vitendo vya askari wa barabarani ambavyo wanavifanya bila weledi,” amesema Rais Samia.
Miongoni mwa Viongozi waliohudhuria hafla hiyo, ni pamoja na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Tulia Akson, Katibu Mkuu Kiongozi na Viongozi wa mbalimbali wa vyombo vya usalama.