Uongozi wa Klabu ya Ihefu FC, umesema hauna mpango wa kubadili Benchi lao la Ufundi kutokana na mafanikio waliyoyapata msimu uliopita 2022/23.

Ihefu FC maarufu ‘Mbogo Maji’ msimu uliopita ilimaliza nafasi ya sita kwenye msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara ikikusanya alama 39, katika michezo 30 iliyocheza.

Katibu Mkuu wa Ihefu FC, Athuman Mndolwa alieleza kuwa wameridhishwa na utendaji wa makocha Zuber Katwila na John Simkoko, hivyo watakachofanya ni kuongeza wachezaji watatu ili kuziba nafasi ambazo zilionesha mapungufu msimu uliopita.

“Malengo yetu msimu unaokuja ni kumaliza ndani ya tano bora na hiyo inatokana na ubora wa benchi letu la ufundi ambalo tumeridhishwa  na utendaji wao na tutaendelea nalo msimu ujao lakini pia tumepanga kuwaongezea wachezaji wengine watatu ili kukiimarisha kikosi chetu,” amesema Mndolwa.

Amesema wamepanga kubakisha asilimia kubwa ya wachezaji wao waliokuwepo msimu uliopita ili kuendeleza kiwango walichokionesha na kufikia malengo yao ya kumaliza msimu ujao ndani ya tano bora.

Bei mpya ya mafuta kutangazwa leo
Zitambue Nchi 11 hatari zaidi Duniani