Uongozi wa Ihefu FC, umesema mchakato wa kumpata kocha mkuu mpya atakayekinoa kikosi chao umefikia hatua nzuri na wanatarajia kumtambulisha kabla ya mzunguko wa kwanza haujamalizika.
Katibu Mkuu wa timu hiyo, Zagalo Chalamila amesema kwa sasa wanakamilisha baadhi ya taratibu ili aweze kusaini mkataba na kuanza kazi kama ambavyo wamekusudia.
“Ni kocha wa viwango, ambaye tunaamini atabadili mwenendo wa timu yetu na kutufikisha kule ambako tumekusudia. Msimu huu tumekusudia kumaliza kwenye nafasi nne za juu,” amesema Chalamila.
Kiongozi huyo amesema kilichowafanya kumleta kocha mpya kabla ya mzunguko wa pili ni kutaka kumpa nafasi ya kutoa mapendekezo yake kwenye usajili wa Dirisha Dogo ambalo linatarajiwa kufunguliwa mwishoni mwa juma hili.
Amesema kocha aliyepita, Moses Basena alishatoa mapendekezo yake kuhusu usajili wa Dirisha Dogo lakini wangependa kusikia na mapendekezo ya kocha wao mpya sababu yeye ndiye atakayekinoa kikosi hicho na kutimiza malengo ambayo wamempa.
Ihefu FC ambayo tayari imefukuza makocha wawili kabla ya mzunguko wa kwanza kumalizika msimu huu, inashika natasi ya 13 ikiwa na idadi kama hiyo ya pointi na mechi walizocheza mnsimu huu.