Taarifa zinaeleza kuwa Uongozi wa Ihefu FC umeachana na Kocha mkongwe wa kimataifa, John Simkoko, wakati timu hiyo ikiwa katika mipango ya kuanza kambi ya kujiandaa na msimu mpya 2023/24.
Ihefu ilianza msimu uliopita chini ya Zubery Katwila kama kocha mkuu kabla ya baadae kutua kwa Juma Mwambusi ambaye hakudumu kwani aliondoka bila sababu kuwekwa wazi, kisha jahazi kupewa Simkoko aliyefukia mashimo na kuifanya timu iwe bora tofauti na ilivyoanza msimu.
Ihefu iliyokuwa inaburuza mkia ilimaliza katika nafasi ya sita ikiwa na alama 39 kutokana na mechi 30, huku ikiweka rekodi ya kuitibulia Young Africans iliyokuwa imecheza mechi 49 bila kupoteza kwa kuifunga mabao 2-1 katika pambano lililopigwa Novemba mwaka jana ‘2022’.
Hata hivyo, habari za ndani zinaeleza, Simkoko ameshamalizana na mabosi wa timu hiyo kwani mkataba wake ulikuwa wa miezi sita pekee.
Alipotafutwa kocha huyo mwenye historia tamu kwenye soka la Bongo alisema uulizwe uongozi juu ya jambo hilo sababu wao ndio wanaujua ukweli kamili.
Kocha Katwila amesema: “Ihefu hatutakuwa na mabadiliko makubwa sababu dirisha dogo la Januari tulifanya usajili wa wachezaji wengi na tuliacha wengi hivyo sahivi ni maandalizi ya kawaida, tutajua nani anaingia na nani anatoka.”