Hatimaye Ikulu ya Korea Kusini imekanusha taarifa zilizosambaa zikidai kuwa kiongozi wa nchi jirani, Korea Kaskazini, Kim Jong-un amefariki dunia au yuko mahututi baada ya kufanyiwa upasuaji wa moyo.
Moon Chung-in ambaye ni Mshauri Mkuu wa Rais wa Korea Kusini, Moon Jae-in kwenye masuala ya sera za nchi za nje, ameiambia CNN kuwa Serikali ya nchi hiyo ina uhakika kuwa Kim Jong-un ni mzima wa afya njema.
“Upande wa serikali yetu uko vizuri, Kim Jong-un yuko hai na ana afya njema. Amekaa katika eneo la Wonsan tangu Aprili 13, 2020. Hakuna mizunguko yoyote isiyo ya kawaida ambayo imeshashuhudiwa,” Moon Jae-in ameiambia CNN.
Tetezi za kuzorota kwa afya ya Kim Jong-un hata kuzushiwa kifo zilianza baada ya kiongozi huyo kutohudhuria sherehe za kumbukizi ya siku ya kuzaliwa ya babu yake, Aprili 15, tukio ambalo hajawahi kutohudhuria.
Shirika la habari la KCNA lilieleza kuwa Kim Jong-un alionekana kwa mara ya mwisho hadharani siku nne kabla ya sherehe hizo, ambapo alihudhuria kikao.
Maafisa wa Marekani walikaririwa na CNN wakieleza kuwa kuna ukweli kuhusu kuzorota kwa afya ya Kim Jong-Un na huenda kweli akawa amefariki dunia, lakini walikiri kuwa imewawia vigumu kupata taarifa za ndani.