Habari njema kwa mashabiki wa Simba SC kuwa beki wao tegemeo, Mkongomani Hennock Inonga hakupata majeraha makubwa na sasa yupo fiti na tayari kucheza mchezo wa Kariakoo Dabi.

Dabi hiyo ya kwanza ya msimu huu ya Ngao ya Jamii ambayo itazikutanisha timu hizo kongwe, mchezo utakaopigwa kesho Jumapili (Agosti 13) kwenye Uwanja wa CCM Mkwakwani mkoani Tanga.

Mkongomani huyo juzi Alhamis (Agosti 10) alishindwa kumalizia mchezo wa Nusu Fainali ya Ngao ya Jamii waliyocheza dhidi ya Singida Fountain Gate na kutolewa katika kipindi cha pili cha mchezo huo baada ya kupata majeraha ya bega.

Akizungumza jijini Tanga Meneja wa Habari na Mawasiliano wa Simba SC, Ahmed Ally amesema kuwa beki huyo hakupata jeraha kubwa litakalomsababishia aikose dabi hiyo.

Ahmed amesema kuwa, bega la beki huyo alipatiwa huduma ya kwanza mara baada ya kutolewa nje na kulirudisha bega lake katika hali ya kawaida.

“Inonga hakupata majeraha makubwa ya bega lake kwenye mchezo dhidi ya Singida Fountain Gate, na hivi sasa anaendelea vizuri kabisa.

“Na atakuwa sehemu ya wachezaji ya watakaocheza dabi hiyo, kama kocha akimuhitaji kumtumia katika mchezo huo ambao ni muhimu kwetu kupata ushindi.

“Akiwa uwanjani hapo madaktari walimpa huduma ya kwanza na kulirudisha bega lake katika hali ya kawaida na anaendelea vzuri,” amesema Ahmed.

Mapinduzi Niger yaiweka njia panda ECOWAS
Jaribio la Wajaluo lakwama Kenya