Beki wa kati kutoka DR Congo Enock Inonga ameuomba radhi Uongozi wa klabu ya Simba SC na wachezaji wenzake, kufuatia utovu wa nidhamu alioufanya wakati wa mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara dhidi ya Coastal Union.
Enonga alioneshwa kadi nyekundu kwenye mchezo huo uliopigwa Uwanja wa Benjamin Mkapa, kufuatia kumpiga kichwa mchezaji wa Coastal Union.
Taarifa zinaeleza kuwa beki huyo amefanya hivyo mbele ya Afisa Mtendaji Mkuu Barbara Gonzalez na viongozi wengine, na kuahidi hatorudia tena, kwani ametambua madhara yake.
Hiyo ni mara ya pili kwa Inonga kuomba radhi, kwani alifanya hivyo saa chache baada ya mchezo dhidi ya Coastal Union uliomalizika kwa sare ya 0-0.
Inonga kwa sasa yupo kambini na timu yake ya Taifa ya DR Congo, kwa ajili ya maandalizi ya mchezo wao wa kufuzu Kombe la Dunia dhidi ya Taifa Stars utakaopigwa leo Alhamis (Novemba 11) Uwanja wa Mkapa jijini Dar.
Kabla ya Inonga kuondoka kambini alilazimika kuwaomba upya radhi Wachezaji na Benchi zima la ufundi lililokuwa sambamba na uongozi wa timu hiyo chini ya Afisa Mtendaji Mkuu Barbara, huku akiahidi kutofanya tena kosa kama hilo.
“Wakati Inonga akiaga kwa ajili ya kujiunga na kikosi chake cha timu ya taifa, alilazimika kuomba radhi kwa mara nyingine kwa wachezaji na Benchi la ufundi, huku akiahidi kutoruhusu hasira za aina hiyo kutokea kiasi cha kusababisha kuigharimu timu kwenye mchezo dhidi ya Namungo baada ya kukosekana.”
“Uongozi kwa pamoja na Benchi la ufundi ulimsamehe, huku ukimtaka kubadilika kweli na kuwa mfano kwa wenzake na endapo siku nyingine atafanya hivyo basi watalazimika kumfungia na kumkata mshahara kabisa,” kimeeleza chanzo cha taarifa hizo kutoka Kambi ya Simba SC.
Kufuatia kosa hilo Kamati ya saa 72 imemuadhibu Inonga kwa kumfungia michezo mitatu sambamba na kumtoza faini ya Shilingi Milioni Moja (1,000,000).