Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasilino ya klabu ya Ruvu Shooting Masau Bwire ameungana na wadau wa soka nchini, kuhamashisha Mashabiki kujitokeza Uwanja wa Benjamin Mkapa kuishangilia Timu ya Taifa ‘Taifa Stars’.

Stars itashuka Dimbani leo Alhamis (Novemba 11) majira ya saa kumi jioni kupambana na DR Congo katika mchezo wa Kundi J, wa kuwania kufuzu Fainali za Kombe la Dunia 2022.

Masau Bwire amehamasisha Mashabiki kwa kuweka andiko la Kizalendo kwenye kurasa zake za mitandao ya kijamii ambapo ameandika:

Hamasa na umoja wetu ni ushindi kwa Taifa Stars

Leo, November 11, 2021, timu yetu ya Taifa, Taifa Stars, inaingia uwanjani na timu ya Taifa ya Congo, kuwania kufuzu fainali za kombe la Dunia, Qatar.

Ni mchezo muhimu mno kwa timu yetu ya Taifa, ni mchezo ambao, ili tuwe na matumaini makubwa ya kusonga hatua nyingine, lazima tushinde.

Uwezo wa timu yetu kushinda inao tena mkubwa, kikubwa ni sisi wananchi, Watanzania, Wazalendo, kuipa ushirikiano na hamasa.

Kwa umoja na wingi wetu, tujitokeze kwa wingi uwanjani, tuishangilie timu yetu, kelele na shangwe zetu, zianikize ushindi katika mchezo huo.
Ushindi kwa timu yetu katika mchezo huo, ni ushinde wetu sisi sote Watanzania, utatuheshimisha kimataifa katika soka.

Serikali yetu ya awamu ya sita, viongozi wetu wa Shirikisho la mpira wa miguu (TFF), wameonesha dhamira ya ushirikiano katika kuhakikisha timu yetu inashinda mchezo wa leo na mingine ijayo, hatimaye, mdogo mdogo, kwa hakika, tunafika Qatar.

Kwa nini Mtanzania, Mzalendo, mwenye nia na mapenzi mema na nchi yako, unayejua nguvu ya umma katika kufanikisha jambo, ushindwe kwenda kwa Mkapa leo, kuishangilia timu ya Taifa lako kuhakikisha tunashinda mchezo wa leo dhidi ya Congo?

Twendeni kwa Mkapa kwa wengi, hamasa yetu, iwatie nguvu na juhudi, ushindi upatikane.
Masau Kuliga Bwire – Mzalendo.
Cc @masaubwire

Zahera: Hautakua mchezo rahisi
Inonga: Sitarudia tena kufanya hili