Jeshi la Iran limeanzisha mashambulizi makali ya makombora Mashariki mwa Syria likilenga kundi la kigaidi linalojiita Islamic States of Iraq and Syria (ISIS).
Kwa mujibu wa jeshi hilo, mashambulizi hayo yaliyofanyika jana ni kulipa kisasi kutokana na shambulizi la kigaidi la Juni 7 katika Bunge la nchi hiyo lililoko Tehran.
Kwa mujibu wa shirika la habari la AP, Iran imeonya kuwa itachukua hatua kama hiyo kwa nchi yoyote ambayo itashambulia sehemu yoyote ya Iran.
Channel 10 ya Israel imekikariri chanzo kimoja cha kiintelijensia kikieleza kuwa makombora hayo yalikuwa na uwezo wa kusafiri umbali wa Kilometa 1,200.
Imeelezwa kuwa hii ni mara ya kwanza kwa Iran kufyatua makombora moja kwa moja kuashiria hali ya vita dhidi ya maadui wake, tangu kumalizika kwa vita kati ya taifa hilo na Iraq mwaka 1988.
Wanaharakati na taasisi za kimataifa zilizoko Syria wanasema kuwa bado hawajapata taarifa kamili ya madhara yaliyotokana na mashambulizi hayo ya Jumapili.
Hivi karibuni, gwaride la kijeshi la Iran lilishambuliwa kwa bomu ambapo taifa hilo lilirusha lawama kwa Marekani na Israel na kuahidi kujibu kijeshi. Marekani na Israel kwa pamoja walikanusha vikali kuhusika na tukio hilo na ISIS ilihusishwa kwa mara nyingine.