Serikali ya Iran imekiri kuhusika kutungua ndege ya abiria ya Ukraine na kusababisha vifo vya watu 176, ikieleza kuwa iliitungua kimakosa baada ya kuhisi ni adui.
Rais wa Ukraine, Hassan Rouhani, leo Januari 11, 2020 ametoa tamko kupitia kituo cha runinga cha taifa hilo, akieleza kusikitishwa na tukio hilo lililoiangamiza ndege hiyo namba 752, Jumatano wiki hii. Rais huyo aliomba radhi familia na wapendwa wote wa waliopoteza maisha.
“Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inaomba radhi na inasikitika kwa kosa hili lililotokea. Mawazo yangu na maombi yangu kwa familia zote zinazoomboleza vifo vya wapendwa wao. Ninatuma salamu zangu za rambirambi kwa dhati,” amesema Rais Rouhani kupitia tamko lake lililowekwa pia kwenye mtandao wa Twitter.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, Javad Zarif ameilaumu Marekani kwa kusababisha kutokea kwa tukio hilo, akieleza kuwa imekuwa siku mbaya kwa Iran na majuto kwa kutungua ndege hiyo kimakosa.
Jeshi la Marekani limeeeleza kuwa ndege hiyo ilifananishwa kimakosa na adui baada ya kugeuka na kuanza kuelekea kwenye eneo nyeti la Jeshi la Mapinduzi la nchi hiyo.
Tukio hilo lilitokea saa chache baada ya Marekani kumuua Kamanda wa Iran, Qassem Soleimani jijini Baghdad nchini Iraq. Iran iliapa kulipiza kisasi na siku chache baadaye ilishambulia kambi mbili za jeshi la Marekani zilizoko nchini Iraq.
Iran ilieleza kuwa shambulio hilo lilisababisha vifo vya wanajeshi 80 wa Marekani, lakini Rais Donald Trump alikanusha akieleza kuwa hakuna aliyepoteza maisha na hakuna aliyejeruhiwa sana.