Iran imetoa waranti wa kukamatwa rais wa Marekani, Donald Trump na imeliomba msaada shirika la polisi ya kimataifa Iterpol kumkamata rais huyo na wengine kadhaa inaoamini walifanya shambulio la ndege isiyo na rubani lililomuuwa jenerali wa juu wa Iran mjini Baghdad.
Mwendesha mashtaka wa Tehran Ali Alqasimehr amesema Trump na watu wengine zaidi ya 30 ambao Iran inawatuhumu kwa kushiriki katika shambulio la Januari 3 lililomuuwa Jenerali Qassem Soleiman mjini Baghdad, wanakabiliwa na mashtaka ya mauaji ya ugaidi.
Alqasimehr hawakuwataja wengine wanaotafutwa mbali ya Trump, lakini amesisitiza kuwa Iran itaendelea kufuatilia mashtaka dhidi yake hata baada ya kukamilika kwa muhula wake wa urais.
Shirika la Interpol lenye makao yake nchini Ufaransa, halikujibu maombi ya kuzungumzia suala hilo.
Ingawa Trump hayuko katika hatari yoyote ya kukamatwa, mashtaka hayo yanaonyesha mzozo unaozidi kati ya Iran na Marekani tangu Trump alipoitoa Marekani kwenye mkataba wa nyuklia kati ya Iran na mataifa makubwa.