Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Dkt. Selemani Jafo amewasilisha bungeni Hotuba ya Mapitio ya Utekelezaji wa Mpango na Bajeti kwa mwaka 2021/22 na Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa mwaka 2022/23.

Akiwasilisha hotuba hiyo leo Aprili 24, 2023, Dkt. Jafo amesema Ofisi ya Makamu wa Rais imekamilisha taratibu zote za kupata Ithibati ya Kitabu ‘Muungano wa Tanganyika na Zanzibar, Chimbuko, Misingi na Maendeleo’ kwa ajili ya kutumika kama kitabu cha ziada kwa shule za sekondari nchini.

Amesema, hatua hiyo itasaidia kuwajengea wanafunzi uelewa kuhusu namna Muungano huu adhimu ulivyoasisiwa pamoja na faida zake ili kuulinda na kuuenzi na kwamba wameendelea kuhimiza umuhimu wa wizara, idara na taasisi zisizo za Muungano kuimarisha ushirikiano na kubadilishana uzoefu, sera, sheria, utaalamu na wataalamu.

Jafo ameongeza kuwa, Ofisi ya Makamu wa Rais imeendelea kuratibu masuala ya Muungano yanayosimamiwa na wizara, taasisi na idara za Muungano kwa faida ya pande zote mbili za Muungano na kuwa kati ya taasisi 33 za Muungano, 27 zina Ofisi Zanzibar na hivyo kusogeza huduma karibu na wananchi.

Dkt. Jafo amesema kutokana na hatua hiyo mafanikio yaliyopatikana ni pamoja na utambuzi na usajili wa wananchi katika mikoa yote ya Tanzania Bara na Zanzibar uliofanywa na Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA) na kutoa ithibati ya mitaala kwa vyuo vikuu vya Tanzania Bara na Zanzibar iliyofanywa na Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU).

Ameyataja mafanikio mengine, kuwa ni Udahili wa wanafunzi wa Shahada ya kwanza katika Vyuo vya Elimu ya Juu Tanzania Bara na Zanzibar kupitia TCU na mafunzo kwa vyuo na shule za sekondari kuhusu Haki za Binadamu na Utawala Bora kwa pande zote za Muungano yaliyotolewa na Tume ya Haki za
Binadamu na Utawala Bora.

Kwa upande wa Hifadhi ya Mazingira, Dkt. Jafo amesema katika kuratibu na kusimamia utekelezaji wa Mpango Kazi wa Uhifadhi wa Bonde la Ruaha Mkuu, Ofisi imeshiriki katika utatuzi wa mgogoro wa ardhi katika Bonde la Mto Ruaha katika eneo la Ihefu ambalo ni chanzo kikuu cha maji kwa Bwawa la Mwalimu
Nyerere.

Aliyempa mwenzake Milioni 118 ajinyonga, aacha ujumbe
Masau Bwire akiri mambo magumu Ruvu Shooting