Mahakama ya katiba nchini Ivory Coast imemuidhinisha rais anayemaliza muda wake Alassane Ouattara, kuwania tena kiti cha urais katika uchaguzi wa urais kwa muhula mwingine.
Aidha, mahakama hiyo hiyo imemzuia rais wa zamani Laurent Gbagbo, na kiongozi wa zamani wa waasi Guillaume Soro kugombea urais katika uchaguzi ujao.
Uamuzi huo umefuatiwa na maandamano yenye ghasia, yanayotishia kuitumbukiza nchi hiyo ya Afrika magharibi katika machafuko kama yale yaliyotokea muongo mmoja uliopita, ambapo maisha ya watu zaidi ya 3000 yaliangamizwa.
Majaji wa mahakama hiyo wameridhia wagombea wanne tu kati ya 44 waliotia nia ya kuwania urais katika uchaguzi mkuu utakaofanyika Oktoba 31.
Miongoni mwa walioruhusiwa kusimama dhidi ya Ouattara no Konan Bedie, rais wa zamani wa Ivory Coast ambaye sasa anao umri wa miaka 86.
Waandamanaji wenye hasira walichoma magari katika miji ya Yopougon na Bangolo, kufuatia makabiliano baina ya wafuasi wa upinzani na maafisa wa usalama.