Siku kama ya leo Aprili 7, mnamo mwaka 1954, huko Victoria Peak, Hong Kong China, alizaliwa mwigizaji nguli na mjasiriamali maarufu duniani Jackie Chan ambaye leo ametimiza umri wa miaka 68.
Kupitia umahiri wake katika michezo ya sarakasi na ucheshi vilimfanya kuwa nyota aliyewavutua wengi waliokuwa wakifuatilia filamu zake kufikia kiwango cha kuwa mmoja wa waigizaji wa kiume wenye idadi kubwa ya mashabiki duniani.
Akiwa na umri wa miaka 7 hadi 17 Chan alisomea sarakasi, uimbaji, karate, na kuigiza, ustadi alioupata huko ulimfanya kuanza kuhusishwa katika filamu akivishwa uhusika wa mtoto mdogo.
Baadae mtayarishaji wa filamu Lo Wei, akitarajia kupata mrithi wa marehemu Bruce Lee, aliamua kukishikilia kipaji cha Chan na kumpa nafasi katika mfululizo wa filamu za kung fu zisizovutia mno, mnamo miaka 1976 – 1978.
Historia yake ya uigizaji kuanzia hapo ilipoanza rasmi, Mpaka sasa Jackie Chan amecheza zaidi ya filamu 150 zikiwamo ‘Police Story’ iliyotoka mnamo mwaka 1985, ‘Dunken Master’ (1994), Project A (1983) pamoja na Dragon Forever (1988) huku akifanikiwa kuchukua tuzo mbali mbali zisizopungua 45.