Kiungo Mshambuliaji ‘Winga’ Jadon Sancho yuko tayari kwa mazungumzo na kocha wa Manchester United, Erik ten Hag, vyanzo vimeiambia ESPN kutokana na mzozo kati ya wawili hao baada ya kufungwa mabao 3-1 na Arsenal.
Sancho alirejea Carrington juzi Jumatatu (Septemba 11) pamoja na wachezaji wengine ambao hawajahusika katika mechi wakati wa mapumziko ya kimataifa.
Itakuwa ni mara ya kwanza kwa mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 23, kukutana ana kwa ana na Ten Hag baada ya uamuzi wake wa kukanusha hadharani madai yaliyotolewa na Mholanzi huyo kwamba alitemwa kwenye mechi ya Arsenal kwa sababu ya kufanya vibaya mazoezini.
Katika chapisho la mtandao wa kijamii ambalo bado liko mtandaoni, Sancho alisema “si kweli kabisa, nimefanya vizuri sana kwenye mazoezi.”
Ten Hag anatarajiwa kufanya uamuzi kuhusu mustakabali wa Sancho baada ya mazungumzo na winga huyo wa zamani wa Borussia Dortmund.
Kwa mujibu wa ripoti hiyo, Man United itaunga mkono chochote ambacho Ten Hag atakiamua.
Chanzo kutoka ndani ya Man United kiliiambia ESPN kwamba hatima ya Sancho itaamuliwa bila ya sababu zingine zozote, pamoja na likizo ya Antony.
Mchezaji huyo wa Kimataifa wa Brazil, Antony amepewa muda na klabu hiyo huku kukiwa na madai ya unyanyasaji alioufanywa kwa wanáwake watatu na hakuna muda wa kurudi kwake.