Mbunge wa wilaya ya Kisarawe Selemani Jafo ameahidi kufanya kazi kubwa zaidi kwa miaka mitano ijayo endapo atapata tena nafasi ya kuteuliwa na Rais John Magufuli katika baraza la mawaziri la mwaka 2020 – 2025.
Jafo ameyasema hayo jijini dodoma wakati akifanya mahojiano na kituo cha habari cha Dar24 kuhusu maoni yake kwa miaka mitano ijayo katika kutumikia wananchi wa Tanzania.
“Tayari nimeshapata jukumu la kwanza la kuwa Mbunge, mengine yote ni mapenzi ya Mwenyezi Mungu na imani ya mheshimiwa Rais Magufuli kwani yeye ndo mwenye jukumu la kuamua nani ataweza kumsaidia kwenye baraza hilo” amesema Jafo.
Akijivunia utendaji kazi wake katika kipindi cha kwanza cha serikali ya awamu ya tano, Jafo amesema wizara yake iliweza kufanya mapinduzi makubwa kwa sekta ya afya kwa kujenga vituo vya afya 487 na hospitali mpya 99 za wilaya, pamoja na ukarabati wa shule kongwe 76.
Aidha, Jafo amejivunia utendaji wake kwa miaka mitano iliyopita kwa kubadilisha miji na manispaa kwa kujenga barabara za lami, masoko na stendi, umeboreshaji na uwasilishaji wa mabaadiliko ya sheria kuhusu wanawake, vijana na watu wenye ulemavu, na utoaji riba ili kuwezesha upatikanaji wa mikopo.