Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Selemani Jafo amelitaka Jeshi la Zimamoto na Uokoaji nchini lishirikiane na Chama cha Skauti Tanzania katika kukomesha majanga yatokanayo na moto kwenye Shule za Msingi na Sekondari.

Jafo ameyasema hayo leo katika makao Makuu ya Jeshi la Zimamoto Tanzania jijini Dodoma, wakati akizindua kampeni ya pamoja kati ya taasisi hizo mbili, huku akitaja kuwa, moja ya sababu zinazochangia kutokea kwa majanga ya moto ni pamoja na kundi la wanafunzi kutokuwa na uelewa wa kutosha juu ya elimu ya majanga.

Amesema majanga ya moto yanapotokea wanafunzi wanapaswa kuwa na maandalizi ya kutosha kielemu kupambana na majanga na hali ya kuzuia yasitokee , hivyo kuanza kwa ushirikiano huo itakuwa ni mwanzo mpya na mzuri katika kupambana na majanga ya moto shuleni.

“Katika siku za hivi karibuni tumeshuhudia baadhi ya shule zikiungua moto na nyingine kuteketea, chanzo kikubwa ukiangalia ni hizi sababu zilizo ainishwa na Kamishna Jenerali wa Jeshi la Zimamoto na uokoaji” amesema Jafo.

Jafo amesema Serikali chini ya Rais Magufuli, inazidi kujenga na kuimarisha miundombinu ya shule nchi nzima, ikiwa ni pamoja na ujenzi wa Shule mpya 1000, hivyo kukamilika kwake lazima kuendane na elimu ya Majanga mbali mbali ikiwemo elimu ya kujikinga dhidi ya moto.

Kuhusu makubaliano baina ya Jeshi la Zimamoto na Uokoaji na Chama cha Skauti Tanzania  kushirikiana katika kutokomeza majanga ya moto shuleni, Waziri Jafo amesema ushirikiano huo unampatia faraja kubwa kwani ana imani, miundombinu inayojengwa sasa hata ile iliyokarabatiwa ya shule kongwe 86 kati ya 89 zilizotumia Shilingi bilioni 89 itatunzwa na kulindwa ipasavyo kutokana na elimu kwa Skauti wanafunzi waliopo shuleni.

Waziri Jafo, amesema Chama cha Skauti Tanzania kimekuwa na jukumu kubwa la kujenga uzalendo miongoni mwa vijana wa kitanzania wawapo shuleni huku akiwataka Maafisa Elimu wa Mikoa na Halmashauri kuendelea kutoa ushirikiano kwa vyama vya Skauti ngazi ya Mkoa na Wilaya, ili uzalendo uliojengeka miongoni mwao uzidi kuimarika.

Akitoa salamu za Jeshi hilo wakati wa hafla hiyo, Kamishna Jenerali wa Jeshi la Zimamoto nchini, John Masunga amesema Jeshi limeanzisha kikosi kazi kwa ushirikiano na Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia na Ofisi ya Rais-TAMISEMI, lengo likiwa ni kuhakikisha elimu dhidi ya majanga ya moto inawafikia wanafunzi lakini kuongeza uelewa wa pamoja juu ya athari za moto miongoni mwao.

Naye Kamishna Mkuu wa Skauti nchini, Mwantumu Mahiza amesema mara zote Skauti wamekuwa wakitekeleza wajibu wao kwa mujibu wa viapo vyao na kuwa wanatambua Serikali inatumia fedha nyingi kwenye uwekezaji wa miundombinu ya shule, kwa mantiki hiyo wao kama Skauti lazima wawe mstari wa mbele katika kuilinda kwa nguvu zote.

IGP awaonya majambazi
Vyama vya siasa vyatakiwa kutoa elimu ya Uraia