Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imepongezwa kwa kupitisha Sheria ya haki ya upatikanaji wa habari kutoka katika taasisi na mashirika ya umma pamoja na binafsi hapa nchini.
Pongezi hizo zimetolewa na Jaji Mstaafu, Amiri Manento ambaye pia aliwahi kuwa Mwenyekiti wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala bora, alipokuwa katika maadhimisho ya siku ya Kimataifa ya Upatikanaji wa Taarifa iliyofanyika katika ukumbi wa Millenium Tower.
“Kwa mujibu wa Katiba kila Mtanzania anayo haki ya kupewa taarifa wakati wowote kuhusu matukio mbalimbali na muhimu kwa maisha ya wananchi kuhusu masuala ya kijamii na kimaendeleo, hivyo mwaka 2016, Sheria ya kupata taarifa ilipitishwa na Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na kuidhinishwa na Rais, John Pombe Magufuli ili kuwezesha wananchi kupata taarifa,” alifafanua Jaji Manento.
Jaji Manento amesema kuwa, hatua ya serikali ya kupitisha Sheria hiyo ni kuendana na mikataba na Sheria za kimataifa ambazo zinamtaka kila mwananchi kutoa, kupokea na kupata taarifa juu ya shughuli mbalimbali zinazoendelea katika taifa lake,Tanzania ni mwanachama na imeridhia Sheria na mikataba hiyo itumike.
Amesema kuwa, Sheria ya kupata taarifa ina umuhimu mkubwa katika taifa kwani zaidi ya nchi 100 duniani zinazotumia sheria hii zimefanikiwa kupambana na vitendo viovu kama vile rushwa, matumizi mabaya ya madaraka kwa viongozi wa umma, ubadhilifu wa rasilimali za nchi, kuongeza uwazi na uwajibikaji kwa viongozi wa umma na taasisi binafsi pamoja na kukuza utawala bora.
Jaji Manento ambaye pia ni mwenyekiti mstaafu wa Tume ya haki za binadamu na utawala bora ametoa wito kwa serikali kuitungia sera na kanuni Sheria hiyo ili ianze kutumika hapa nchini mara moja.
“Ningependa kuwakumbusha watumishi wa serikali hasa wale wanaohusika na utekelezaji wa Sheria hii, kuchukua hatua mahususi kuhakikisha kuwa kanuni zinatayarishwa na zinatagazwa kwenye gazeti la serikali,”amesisitiza.