Wasimamizi wa Uchaguzi nchini, wametakiwa kufanya kazi kwa weledi na kuzingatia Katiba, Sheria, Kanuni na maelekezo ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi wakati wote wanapotekeleza majukumu yao.
Hayo yamesemwa hii leo Juni 19, 2023 jijini Tanga na Makamu Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi, Jaji wa Mahakama ya Rufaa, Mbarouk Salim Mbarouk wakati akifungua mafunzo ya Wasimamizi na Wasimamizi Wasaidizi wa Uchaguzi ngazi ya Jimbo na Kata.
Amesema, “jambo muhimu mnalotakiwa kuzingatia ni kujiamini na kufanya kazi kwa weledi, mnapaswa kuzingatia Katiba ya Nchi, Sheria za Uchaguzi na Kanuni zake, Maadili ya Uchaguzi na Maelekezo mbalimbali yanayotolewa na yatakayotolewa na Tume katika kipindi hiki cha uchaguzi mdogo.”
Jaji Mbarouk pia amewaasa washiriki hao wa mafunzo kuhakikisha kuwa pamoja na uzoefu ambao baadhi yao wanao katika uendeshaji wa uchaguzi, wahakikishe wanazingatia maelekezo watakayopewa na Tume badala ya kufanya kazi kwa mazoea.
Aidha, amewataka watendaji hao wa uchaguzi kuvishirikisha vyama vya siasa na wadau wengine wa uchaguzi katika maeneo yao kuhusu masuala mbalimbali ya kiuchaguzi ambayo wanastahili kushirikishwa ili kurahisisha utendaji wa kazi.
Kata zilizotarajiwa kufanya uchaguzi mdogo ni pamoja na Ngoywa iliyopo Halmashauri ya Wilaya ya Sikonge, Kalola iliyopo Halmashauri ya Wilaya ya Uyui, Sindeni iliyopo Halmashauri ya Wilaya ya Handeni, Potwe iliyopo Halmashauri Manispaa ya Muheza.
Zingine ni Kwashemshi iliyopo Halamshauri ya Wilaya ya Korogwe, Bosha iliyopo Halmashauri ya Wilaya ya Mkinga, Mahege iliyopo katika Halmashauri ya Wilaya ya Kibiti na Bunamhala iliyopo katika Halmashauri ya Mji wa Bariadi.
Zizpo pia kata za Njoro na Kalemawe zilizopo katika Halmashauri ya Wilaya ya Same, Mnavira iliyopo katika Halmashauri ya Wilaya ya Masasi, Kinyika iliyopo katika Halmashauri ya Wilaya ya Makete, Magubike iliyopo katika Halmashauri ya Wilaya ya Kilosa na Mbede iliyopo katika Halmashauri ya Wilaya ya Mpimbwe.