Nyota wa zamani wa klabu za Simba SC (Tanzania) na Kaizer Chief (Afrika Kusini) James Agyekum Kotei amesaini mkataba mpya na Klabu ya Singida Bog Stars itakayoshiriki kwa mara ya Kwanza Mshike Mshike wa Ligi Kuu Tanzania Bara msimu ujao.
Kotei amesaini mkataba mpya wa Klabu hiyo, baada ya kuwa sehemu ya kikosi cha DTB kwa sasa Singida Big Stars msimu uliopita, na kuiwezesha kupanda Ligi Kuu Tanzania Bara.
Kiungo huyo alianza mazungumzo na Uongozi wa Klabu hiyo, baada ya kuibuka kwa tetesi za kutakiwa na klabu nyingine za nchini kwao Ghana, hasa aliporejea nyumbani kwa ajili ya mapumziko.
“Amerudi na ameanza mazoezi na wenzake, ni mchezaji mzuri ambaye alitusaidia hadi tunapanda ligi kuu hivyo tuliona ni vizuri kumshawishi tukiamini uzoefu wake utaleta manufaa kwenye kikosi chetu,” kilisema chanzo hicho.
Akizungumzia hilo, Kotei amesema amefurahia kurejea tena Tanzania akiamini ni sehemu nzuri na yenye ligi ya ushindani.
“Nimefurahi kuungana na Said Ndemla kwenye kikosi chetu baada ya awali kucheza naye tukiwa Simba, tumeishi kama ndugu kwa kipindi kirefu na kucheza tena pamoja naamini tutafanya makubwa msimu ujao,” amesema Kotei.
Kotei aliyeichezea Simba kwa misimu miwili kuanzia 2017-2019 alitua nchini mwishoni mwa Juma Lililopita kukamilisha dili hilo kisha kuungana moja kwa moja na kikosi hicho jijini Arusha kilichoweka kambi ya kujiandaa na maandalizi ya msimu (pre season).