Washirika wa kibiashara wa Marekani, wanaoongozwa na mataifa yenye nguvu kiuchumi katika bara la Asia, China na Japan hii leo wamepinga uamuzi wa mpango mpya wa utozaji ushuru kwa bidhaa za chuma cha pua na bati zinazoingizwa Marekani uliosainiwa na Rais, Donald Trump.
Hayo yanajiri wakati ambapo kuna ongezeko kubwa la wasiwasi kuhusu kuibuka kwa vita vya kibiashara.
Japan ambaye ni mshirika wa karibu wa Marekani imeonya kuhusu 25% ya ushuru kwa bidhaa za chuma cha pua na 10% kwa bati kuwa zinaweza kuwa na matokeo makubwa katika mahusiano ya kibiashara kati ya mataifa hayo yenye nguvu kubwa kiuchumi.
Japan kupitia waziri wake wa mambo ya nje, Taro Kono imeshutumu hatua hiyo kwa kusema itakuwa na matokeo makubwa kwenye ushirikiano wa kibiashara na uchumi wa dunia kwa ujumla.
Rais wa Marekani Trump amesema, ushuru huo mpya utakaoanza kutekelezwa baada ya siku 15, kwanza hautazigusa Canada na Mexico.
Hata hivyo, Marekani imesema kwa nchi ambazo ni washirika wa karibu wa masuala ya usalama na biashara zinaweza kufanya mashauriano ya kusamehewa.