Mwalimu mmoja wa shule nchini Marekani alifanikiwa kutumia saa tano kujitenga kwa hiari kwenye choo cha ndege baada ya kupimwa na kukutwa na maambukizi ya uviko 19 katikati ya safari ya ndege.
Kwa mujibu wa shirika la habari la NBC Marisa Fotieo anasema alihisi koo lake likimuuma alipokuwa akisafiri kutoka Chicago kwenda Reykjavik, Iceland, tarehe 20 Desemba.
Fotieo amesema alifanya kipimo cha haraka kwa kifaa alichokuja nacho, ambacho kilithibitisha kuwa alikuwa ameambukizwa na alibaki chooni kwa muda wote uliosalia wa safari, huku mtumishi wa ndege akimpa chakula na vinywaji.
Hata hivyo haikuwekwa wazi mara moja ikiwa alilazimika kuwasilisha kipimo cha Covid-19 kabla ya kupanda ndege.
“Ilikuwa tukio la kichaa. Kulikuwa na watu 150 kwenye ndege, na hofu yangu kubwa ilikuwa kuwaambukiza.” Fotieo, aliambia NBC News.
Video aliyochapisha kwenye Tiktok akiwa ndani ya choo cha ndege ya Icelandair imetazamwa zaidi ya mara milioni nne na ametumia ukurasa huo kumsifu mhudumu wa ndege kwa kumsaidia wakati wa tukio hilo.
“Alihakikisha kuwa nina kila kitu nilichohitaji kwa saa tano zilizofuata kutoka kwa chakula hadi vinywaji na mara kwa mara aliniangalia na kunihakikishia kuwa nitakuwa sawa,” aliongeza.
Fotieo alisema alipowasili Iceland ilimbidi kujitenga katika hoteli ya Msalaba Mwekundu.
Masaibu yake yamekuja kukiwa na kuenea kwa aina mpya ya kirusi cha Omicron, ambayo inaendelea kuchochea kuongezeka kwa kesi mpya za maambukizi kote nchini Marekani.
Kulingana na Kituo cha Kudhibiti na Kuzuia Magonjwa Marekani kwa wastani wa siku saba wa kesi mpya ni 277,000, kiwango cha juu zaidi tangu kuanza kwa janga hilo ikiwa viwango vya vifo na kulazwa hospitalini, vinaendelea kuwa sawa.
Idadi hiyo inayoongezeka ya watu wanaolazimika kujitenga kwa sababu ya maambukizo imeweka shinikizo kwa tasnia kadhaa, pamoja na usafiri wa anga.