Mshambuliaji kutoka DR Congo Jean Othos Baleke bado anaamini Simba SC ina nafasi kubwa ya kusonga mbele kwenye MIchuano ya Ligi ya Mabingwa Barani Afrika msimu huu 2022/23.
Simba SC tayari imepoteza michezo miwili ya Hatua ya Makundi ikifungwa 1-0 na Horoya AC ya Guinea katika mchezo wa kwanza mjini Conakry, kisha ikapoteza 3-0 nyumbani Dar es salaam dhidi ya Raja Casablanca ya Morocco.
Baleke ambaye amesajiliwa Simba SC kwa mkopo wa mwaka mmoja akitokea TP Mazembe, amesema matokeo ya michezo hiyo hayapaswi kuwatakatisha tamaa Mashabiki na Wanachama wa Mnyama badala yake wanatakiwa kuendelea kuwa sambamba na timu yao, kuelekea mchezo wa Mzunguuko watatu dhidi ya Vipers SC.
“Nadhani ni wakati wa kutuunga mkono wa sababu bado tuna nafasi ya kufanya vizuri katika michezo iliyosalia, kila mchezaji amekuwa kwenye wakati mgumu juu ya matokeo ya mchezo uliopita ambao matarajio yetu yalikuwa ni kupata ushindi.”
“Kitu kikubwa ni mashabiki kuendelea kutopa sapoti wakati wote ili kuweza kupata ushindi kwenye mchezo wetu ujao dhidi ya Vipers SC kwa sababu kila mchezaji matarajio yake ni kuona tunaweza kufika hatua kubwa katika michuano hii ingawa tumekuwa na matokeo ya kushangaza kwenye michezo yetu miwili iliyopita.” amesema Baleke
Kikosi cha Simba SC kitacheza dhidi ya Vipers SC Jumamosi (Februari 25) mjini Entebe-Uganda katika Uwanja wa St Merry’s, huku kikipoteza michezo miwili ya awali dhidi ya Horoya AC (Guinea) na Raja Casablanca (Morocco).