Mchambuzi wa Soka nchini Tanzania Jemedari Said amewashukia baadhi ya Wadau wa Soka wanaohoji kwa mtazamo hasi, kuhusu Simba SC kucheza na Timu ya Dhafra FC inayoshika nafasi ya mwisho katika Msimamo wa Ligi ya Falme za Kirabu ‘UAE PRO League’.
Jana Jumanne (Januari 10) Simba SC ilithibitisha kucheza michezo miwili ya Kirafiki, ikiwa kambini Dubai-Falme za Kiarabu ilipoweka kambi ya kujiandaa na Mshike Mshike wa Ligi ya Mabingwa Barani Afrika na Ligi Kuu Tanzania Bara chini ya Kocha Robertinho.
Akizungumza mapame leo Jumatano (Januari 11) kupitia Kipindi cha Sports HQ, Jemedari amesema: “Nimeona watu wakihoji kwa nini Simba wanacheza na timu inayoshika nafasi ya mwisho katika Ligi Kuu ya Dubai.”
“Kuna hatua za mechi mkiwa katika maandalizi, hii mechi ambayo itamfanya kocha mpya kuona kile alichokifundisha kwa siku kadhaa kimewafikaje wachezaji wake.”
“Kama tunaamini timu ya mwisho Dubai, haitoshi kucheza na Simba, basi hii ni timu sahihi kwa Simba. Wakitoka hapo watacheza na CSKA Moscow ina maana hapo ushindani wa mechi umepanda “
Simba SC itaanza kucheza dhidi ya Dhafra FC keshokutwa Ijumaa (Januari 13) saa kumi jioni kwa saa za Afrika Mashariki, kisha itapambana na mabingwa wa zamani wa UEFA Europa League klabu ya CSKA Moscow kutoka nchini Urusi Jumapili (Januari 15) saa saa kumi jioni kwa saa za Afrika Mashariki.