Baada ya Jeshi la Sudan kumng’oa madarakani Rais wa taifa hilo, Omar al-Bashir, limetangaza hali ya hatari katika kipindi cha miezi mitatu, huku likisema litaongoza katika kipindi cha miaka miwili mfululizo.
Akitangaza uamuzi wa kuing’oa serikali ya Al-Bashir madarakani jana tarehe 11 Aprili 2019 kupitia televisheni ya taifa ya Sudan, Waziri wa Ulinzi Sudan, Ahmed Awad Ibn Auf amesema jeshi la nchi litaongoza katika kipindi cha miaka miwili cha mpito.
Ibn Auf amesema Al-Bashir amekamatwa na Jeshi na kuwekwa katika sehemu salama, huku mipaka ya taifa hilo ikifungwa.
“Nitangaza kama Waziri wa Ulinzi kung’oa utawala na kumweka kiongozi wake katika sehemu salama,” amesema Ibn Auf.
Waziri huyo wa masuala ya ulinzi nchini Sudan amesema katika kipindi cha miaka miwili cha uongozi wa jeshi, taifa hilo litafanya mchakato wa kurekebisha katiba yake, ili kuandaa mazingira mazuri ya ufanyikaji wa uchaguzi huru na wa haki.
Ibn Auf amesema katika utawala wa jeshi, haki za binadamu zitaheshimiwa.
Hatua hiyo ya Jeshi nchini Sudan kung’oa utawala wa al-Bashir umekuja baada ya maandamano ya amani ya wananchi yaliyofanyika miezi kadhaa, kushinikiza rais huyo aliyedumu madarakani kwa miaka 30 kuachia ngazi.
Baada ya Jeshi kutangaza hatua hiyo, maelfu ya wananchi wa Sudan walitamalaki katika mji mkuu wa nchi hiyo, Khartoum wakishangilia Al-Bashir kuondolewa madarakani.