Jeshi la Zimbabwe limetumia kituo cha habari cha Taifa (ZBC) kueleza lengo la kuingiza mitaani silaha nzito za kivita ikiwa ni pamoja na vifaru.

Jeshi hilo ambalo lilichukua hatua hiyo saa chache baada ya kuviambia vyombo vya habari kuwa halitasita kuingilia kati mgogoro wa madaraka ndani ya chama tawala cha Zanu-PF baada ya Rais Mugabe kumfukuza aliyekuwa Makamu wa Rais, Emmerson Mnangagwa limesema hatua hiyo imelenga kuwasaka wahalifu na sio vinginevyo.

Kupitia tamko lake kwa vyombo vya habari, jeshi hilo limesisitiza kuwa hakukuwa na mpango wa kufanya mapinduzi ya kijeshi na kwamba Rais Mugabe na familia yake wako salama na walikuwa wanajua kinachoendelea.

Hata hivyo, hawakuainisha ni walafu gani waliokuwa wanasakwa ndani ya nchi hiyo na silaha nzito za kivita.

“Tungependa kulihakikishia taifa kuwa mheshimiwa Rais na familia yake wako salama na ulinzi wao ni wa uhakika,” limeeleza tamko lililosomwa na Meja Generali, Gen Sibusiso Moyo.

“Tunalenga wahalifu wanaomzunguka ambao wanapanga matendo ya kihalifu, ambao wanasababisha mateso ya kijamii na kiuchuni nchini. Punde tutakapokamilisha mkakati wetu, hali ya kawaida itarejea,” aliongeza.

Kutokana na vitendo hivyo vya jeshi, Balozi za Marekani na Uingereza zilitoa tamko kwa raia wake waliopo nchini humo, zikiwataka kutotoka nje ya nyumba zao hadi hadi hali itakaporejea kwenye ukawaida.

Rais Mugabe alimfuta kazi Mnangagwa kwa madai kuwa anapanga njama  za kumhujumu na kutaka kumrithi bila kufuata taratibu za kichama. Alisema Mnangagwa amekuwa akienda kwa waganga na watabiri akitaka kujua Mugabe atakufa lini.

Kutokana na hatua hiyo ya Mugabe, Mkewe mama Grace anatajwa kuwa na nafasi kubwa zaidi ya kurithi nafasi ya mumewe.

LIVE: Yanayojiri Bungeni Dodoma leo Novemba 15, 2017
Video: Argentina yachezea kichapo, Aguero apoteza fahamu