Jeshi la Zimbabwe limeonya kuingilia kati mgogoro unaoendelea kati ya viongozi wa chama tawala cha ZANU-PF, baada ya Rais Robert Mugabe kumfukuza kazi aliyekuwa Makamu wa Rais, Emmerson Mnangagwa.
Kamanda wa Jeshi la Zimbabwe, Jenerali Constantino Chiwenga amefanya mkutano na vyombo vya habari akiwa na viongozi wengine waandamizi 90 wa jeshi hilo na kutoa onyo hilo.
Amesema endapo wapigania uhuru wataendelea kugombana kuhusu madaraka, jeshi hilo halitasita kuchukua hatua.
“Kung’olewa madarakani kunakoendelea sasa, ambako kwa uwazi kunalenga wajumbe wa chama ambao walipigania uhuru, lazima kusitishwe,” alisema Jenerali Chiwenga.
“Tunawakumbusha wanaofanya hivi kuwa katika masuala ya kulinda mapinduzi yetu, jeshi halitasita kuingilia kati,” aliongeza.
Rais Mugabe alimfukuza kazi Makamu wake wa Rais akieleza kuwa amekuwa akiendesha kampeni ya chinichini ya kutaka kumrithi bila kufuata utaratibu wa chama.
Pia, alidai kuwa Mnangagwa alienda kwa watabiri na waganga akitaka kujua ni lini Mugabe atafariki dunia.
Inaaminika kuwa baada ya Mnangagwa kuondolewa, mke wa Rais Mugabe, Mama Grace ndiye anapewa nafasi zaidi ya kurithi kiti cha urais kwa tiketi ya ZANU-PF.