Kiongozi wa Kamati ya Mamlaka ya Ushirikiano wa Serikali za Afrika Mashariki na Pembe ya Afrika – IGAD na Rais wa Kenya, William Ruto ameongoza ujumbe wake kujadili juu ya uwezo wa kupelekwa kikosi cha dharura cha kikanda na kuanzisha mazungumzo baina ya pande mbili kinzani ili kudumisha amani ya Sudan, huku Jeshi la Serikali likimkataa kama mpatanishi.

Akifungua mkutano Ruto amesema, “Mkutano huu lazima ufungue njia ili kuweza kupatikana makubaliano yasiyo na masharti ya kusitisha mapigano ambayo yataruhusu kuwasilishwa kwa msaada wa dharura bila ya pingamizi yoyote, kuhakikisha usalama wa raia, kusitisha uharibifu wa mali na miundombinu pamoja na kukomesha mauaji ya binadamu, na hivyo kuwawezesha wasudan kupata huduma za kijamii.” 

Kiongozi huyo wa Kenya, amependekeza masuala matatu muhimu ili kuweza kurudisha amani nchini Sudan ikiwemo kuruhusu msaada wa dharura kufika kila mahala bila ya vizuizi, pili kuanzisha maungumzo ya moja kwa moja kati ya viongozi wa jeshi la Sudan na kikosi cha RSF, na tatu kupanga mazungumzo ya kitaifa yatakayowahusisha watu wote ili kutayarisha mpito wakati wa kuelekea njia ya demokrasia.

Hata hivyo Serikali ya kijeshi ya Sudan haijapeleka ujumbe wake huko Addis Ababa ikisema kwamba ombi lao la kumondoa rais Ruto kama mpatanishi halijatiliwa maanani ingawa Kikosi cha Wapiganaji cha msaada wa dharula -RSF, kilihudhuria.

Viongozi hao, walikutana jijini Addis Ababa nchini Ethiopia, akiwepo Waziri wa mambo ya nje wa Djibouti, Somalia na Uganda, wajumbe wa Marekani, Umoja wa Mataifa na Serikali ya mpito ya kiraia ya Sudan iliyopinduliwa na wanajeshi, wote wametaka pande zote mbili kusitisha mapigano na kuanza mazungumzo ya amani.

Fabrice Luamba Ngoma asubirishwa Simba SC
Habari Kuu kwenye magazeti ya leo Julai 11, 2023