Maafisa wa jeshi wa Cameroon wamesema wamepata kaburi la halaiki karibu na mpaka wa Nigeria, likiwa na miili ya raia 9 wakiwemo maafisa 5 wa serikali, ambao walitekwa nyara na waasi Juni 2021.
Maafisa hao wamesema walielekezwa kwenye kaburi hilo na mpiganaji wa uasi aliyeshiriki mauaji hayo baada ya kujisalimisha na kujiunga na kituo cha upokonyaji silaha na urekebishaji tabia.
Aidha, Jeshi la Cameroon limesema walifukua miili kutoka kwenye kaburi hilo lililopo umbali wa takriban kilomita 20 kutoka mji wa Ekondo Titi ambao unapatikana kwenye eneo la kiutawala la Ndian karibu na mpaka wa Nigeria.
Miili iliyopatikana ilisafirishwa kwa kutumia magunia kutoka kwenye msitu na kwa muda sasa waasi wamekuwa wakidai kuhusika katika utekaji nyara wa maafisa hao, kwa madai kwamba walikuwa wanashirikiana na Serikali kuu kuwadhohofisha.