Jimbo la Missouri la Marekani limefungua mashtaka dhidi ya Serikali ya China kwa madai kuwa haikufanya jitihada za kutosha kudhibiti kusambaa kwa virusi vipya vya corona (Covid-19).
Katika shtaka hilo, Mwanasheria Mkuu wa jimbo hilo, Eric Schmitt ameeleza kuwa kutofanyika kwa jitihada za kutosha nchini China na kusambaa kwa covid-19 kumesababisha jimbo lake kuathirika kwa kiasi kikubwa ikiwa ni pamoja na kupoteza mabilioni ya dola za kimarekani katika uchumi wake.
“Hapa Missouri, athari za virusi vya corona ni kubwa sana na halisi – maelfu wameathirika na wengine wamepoteza maisha, familia zimetengana na kupoteza wapendwa wao, biashara ndogo zimefungwa na wanaoishi kwa kutegemea kipato cha kila siku wanahangaika kuweka chakula mezani,” amesema Bw. Schmitt.
“Serikali ya China iliidanganya dunia kuhusu hatari na asili ya COVID-19, iliwanyamazisha watoa taarifa na ikafanya juhudi kidogo na zisizoridhisha kuhakikisha inazuia kusambaa kwa virusi, ni lazima wawajibike,” BBC inamkariri Mwanasheria Mkuu, Schmitt.
Kesi hiyo imefunguliwa Jumanne, Aprili 21, 2020 dhidi ya Serikali ya China, Chama cha Kikomunisti cha China (Chinese Communist Party) na maafisa wa China na taasisi zake.
Hata hivyo, wataalam wa masuala ya sheria wanatilia shaka mwenendo wa mashtaka hayo. Sheria inaipa kinga kubwa Serikali ya nje ya Marekani kushtakiwa ndani ya mahakama za Marekani.
China ilitangaza kugundua maambukizi ya virusi vipya vya corona nchini humo Desemba mwaka jana, ikiwa ni taifa la kwanza kuvibaini.