Mikoa ya kanda ya Kaskazini mwa Tanzania, imetajwa kuongoza kwa matatizo ya moyo yanayosababishwa na bakteria kwa Jina la kitaalamu ‘Rheumatic heart disease’.
Daktari Bingwa wa Moyo na Mkuu wa Idara ya moyo ya watu wazima, kutoka Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI), George Longopa ameyasema hayo katika mahojiano Maalumu na Dar24 Media kuzungumzia siku ya Moyo Duniani.
“Kwa tafiti chache ambazo zimefanyika zimeonesha kuna baadhi ya watu ambao Valve zao zimeziba, zile zinazoruhusu damu kutoka chumba kimoja kwenda kingine, wengi wanatokea mkoa wa Manyara,” amesema Dkt. Longopa.
Ameongeza kuwa, “watafiti wameendelea kuhusianisha mazingira ya watu wa kaskazini na maisha yao ya kitamaduni kwa nini Mikoa ya Manyara na Arusha kwa sababu bacteria hawa wanapatikana nchi nzima sasa ukiangalia ni kwa nini wale wa kule labda ni kwa sababu ya mazingira yao wanayoishi ukiangalia kulala na Ng’ombe, na vinginevyo,”
Dkt. Longopa amewashauri watafiti kuendelea kufanyia kazi suala hilo ili kuja na jibu kamili za sababu za kwa nini wananchi wa Mikoa hiyo wanaongoza kwa matatizo hayo ili kuwashauri kufanya maamuzi sahihi juu ya moyo yao.
Amesema, katika kuadhimisha siku ya Moyo taasisi ya JKCI pamoja na Hospitali ya Serian Arusha wameshirikiana kwa wiki nzima kufanya upimaji kwa Wananchi bure ili kuendelea kuwabaini Wananchi wenye matatizo ya moyo mapema na kuwapa ushauri wa kufuata ili kupata tiba.
Mapema hivi karibuni, Mkuu wa idara ya utafiti na mafunzo na Daktari bingwa wa magonjwa ya moyo wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI), Peter Kisenge alisema watu 791 wamefanyiwa uchunguzi na kupata matibabu katika kambi maalum ya matibabu ya moyo inayofanyika katika hospitali ya Arusha Lutheran Medical Centre (ALMC).
Dkt. Kisenge alisema, wengi wa watu hao walikutwa na matatizo mbalimbali ya moyo huku asilimia 25 wakiwa na tatizo la shinikizo la juu la damu katika kambi hiyo ya siku tano iliyoanza tarehe 26 na itamalizika tarehe 30 mwezi huu kati ya Wataalamu wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI), kwa kushirikiana na Arusha Lutheran Medica Centre..
“Tumewafanyia pia uchunguzi watoto ambapo wengine tumewakuta na matatizo ya valvu za moyo na matatizo ya moyo ya kuzaliwa nayo ambayo ni matundu na mishipa ya damu ya moyo kutokukaa katika mpangilio wake hawa nao tumewapa rufaa ya kuja kutibiwa JKCI”, alisema Dkt. Kisenge.
Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete, itaendelea kuwasogezea wananchi huduma za kibingwa za matibabu ya moyo kwa kuwafuata mahali walipo, na kuwajengea uwezo wataalamu wa afya wa jinsi ya kutambua na kutibu magonjwa ya moyo, kwani Serikali imenunua mashine za kisasa za kuchunguza moyo na kuzisambaza katika Hospitali mbalimbali nchini.
Maadhimisho ya siku ya moyo duniani, yanafanyika katika Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete Septemba 29, 2022 kwa kufanya upimaji wa magonjwa mbalimbali bure, na Kauli mbiu ya siku hiyo inasema “Fanya uamuzi sahihi kuhusu Moyo wako.”