Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasilino wa Klabu ya Young Africans Ally Kamwe amesisitiza ushindi kwenye mchezo wa Mkondo wa Kwanza wa Ligi ya Mabingwa Barani Afrika dhidi ya Al Hilal ya Misri.

Young Africans itaikaribisha Al Hilal Jumamosi (Oktoba 08), Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es salaam, kisha itakwenda mjini Khartoum-Sudan kwa ajili ya mchezo wa mkondo wa pili kati ya Oktoba 14-16.

Akizungumza katika kipindi cha Sports Arena cha Wasafi FM, Ally Kamwe amesema Uongozi, Benchi la Ufundi pamoja na Wachezaji wamejiandaa kikamilifu kuelekea pambano hilo, huku ari ya ushindi ikiendelea kuongezeka siku hadi siku.

Amesema malengo makubwa ni kushinda mchezo huo kwa matokeo ya jumla (Nyumbani na Ugenini), ili kutimiza lengo la klabu hiyo kongwe katika ukanda wa Afrika Mashariki na kati ya kutinga hatua ya Mkundi na baadae kucheza Robo Fainali.

“Malengo makubwa ya Young Africans ni kucheza Robo Fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika. Kama una malengo hayo halafu unaihofia Al Hilal utakuwa unachekesha”

“Siamini kama timu ya Al Hilal inapaswa kuipasua kichwa Young Africans, tayari Young Africans ni timu kubwa sana. Hatua ambayo wanapitia Al Hilal [kutengeneza timu], Young Africans ilishapita miaka minne nyuma”

“Sisi tayari tuna wachezaji wazuri na tuna timu nzuri, wenzetu wana wachezaji wazuri wanajitafuta kutengeneza timu nzuri. Young Africans sio timu ya kuumiza kichwa kuifikiria Al Hilal” amesema Ally Kamwe

Al Hilal ilisonga mbele katika Michuano ya Ligi ya Mabingwa Barani Afrika kwa faida ya bao la ugenini dhidi ya Mabingwa wa Soka wa Ethiopia St George, ikitanguliwa kufungwa 2-1 ugenini na kushinda nyumbani Khartoum-Sudan 1-0.

Young Africans ambayo ndio Bingwa wa Tanzania Bara, ilisonga mbele kwenye Michuano hiyo kwa kuibamiza Zalan FC kutoka Sudan Kusini kwa matokeo ya jumla 9-0. Ikishinda 4-0 kwenye mchezo wa Mkondo wa Kwanza, kisha ikashinda 5-0 katika mchezo wa Mkondo wa Pili.

Waandishi wa habari, Mashabiki wanyooshewa kidole
Mikoa ya kaskazini kinara tatizo la Moyo